Bashungwa akabidhiwa ofisi na Masauni, Wizara Mambo ya Ndani

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa amekabidhiwa ofisi na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Mhandisi Hamad Masauni ambaye sasa ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), leo Desemba 13 jijini Dodoma.

Makabidhiano hayo yamefanyika baada ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan kuwaapisha Mawaziri hao Desemba 10, Tunguu Zanzibar.

Advertisement

Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Waziri Bashungwa amemshukuru mtangulizi wake kwa makabidhiano ambayo yatakuwa mwongozo wa kusimamia na kutekeleza majukumu yaliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani Nchi.

SOMA: Bashungwa ataka umoja viongozi Kagera

Sambamba na hilo, Waziri Bashungwa amemshukuru Rais Dk Samia ambapo amesema, “Niendelee kumshukuru Rais wetu na nimuahakikishie kama ambavyo alituelekeza wakati anatuapisha kwamba niendeleze pale ulipoishia Waziri Masauni.”

Aidha, Bashungwa amesisitiza suala la Watumishi wa Wizara na vyombo vyake vya usalama kufanya kazi kwa kushirikiana ili kwa pamoja kusimamia na kutekekeleza majukumu yao kikamilifu.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamadi Masauni amesema Waziri Bashungwa anaipokea Wizara ikiwa katika hali nzuri na hali hiyo inatokana na namna Rais Dk Samia alivyoiwezesha kibajeti Wizara hiyo.

“Mheshimiwa Rais amefanya kazi kubwa sana miongoni mwa kazi aliyoifanya ni kuiwezesha Wizara kuwa na uwezo wa kutekeleza zaidi majukumu yake.” amesema Waziri Masauni.

Waziri Masauni ameeleza kuwa Wizara inaendelea na utekelezaji wa maelezeko ya Tume ya Haki Jinai ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wananchi wanahudumiwa kwa haki, bila uonevu wala dhuluma.

Makabidhiano hayo yameshuhudiwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo pamoja na Naibu Katibu Mkuu, Dk Maduhu Kazi.