Bashungwa ataka changamoto ajira mpya za walimu zianikwe
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa amemwagiza Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu, Dkt. Charles Msonde kufuatilia malalamiko na changamoto zote zinazowakabili walimu wa ajira mpya 9,800 ili ziweze kufanyiwa kazi.
Katika taarifa yake kwa vyombo vya Habari, Bashungwa amesema amekuwa akipokea malalamiko mengi kutoka wa walimu wa ajira mpya zilizotolewa na Serikali mwezi Juni, 2022 ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa baadhi ya wilaya ambazo hazijatoa fedha za kujikimu kwa walimu hao.
Aidha, Bashungwa ameagiza kutolewa kwa ufafanuzi wa viwango vya malipo kwa mujibu wa tararibu na vigezo vinavyotumika katika malipo hayo ili kuondoa sintofahamu ambazo zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara.
Bashungwa amesema serikali ya awamu ya sita ni sikivu na itaendelea kusikiliza na kutatua changamoto watakazokumbana nazo Wakati wakitekeleza majukumu ya kuwafundisha wanafunzi.
Ikumbukwe kuwa Juni 26, 2022 Serikali ilitoa ajira za kada za ualimu kwa waombaji wenye sifa waliokidhi vigezo 9,800 ambapo walimu 5,000 wamepangwa shule za msingi na walimu 4,800 shule za sekondari.