Bei za mbuzi zapanda Dar

WAKATI Waislamu duniani wakijiandaa kuadhimisha Sikukuu ya Eid al-Adha inayohusisha ibada ya kuchinja wanyama, wafanyabiashara wa mifugo katika Soko la Vingunguti jijini Dar es Salaam wamesema biashara ya mbuzi mwaka huu imekumbwa na ushindani mkubwa pamoja na kupanda kwa gharama za biashara.

Akizungumza na Daily News Digital, mmoja wa wauzaji wa mbuzi katika soko hilo alisema tofauti na miaka iliyopita, mwaka huu idadi ya wauzaji imeongezeka katika maeneo mbalimbali ya jiji hali iliyopunguza wateja wanaofika Vingunguti.

“Miaka iliyopita watu wengi walikuwa wanakuja hapa Vingunguti kununua mbuzi, lakini sasa karibu kila eneo kuna wauzaji hivyo ushindani umeongezeka na biashara imekuwa ngumu kidogo,” alisema mfanyabiashara huyo.

Wauzaji hao pia walieleza kuwa bei ya mbuzi imeongezeka kutokana na gharama kubwa za ununuzi kutoka kwa wafugaji wa mikoani pamoja na kupanda kwa gharama za usafirishaji zinazochangiwa na ongezeko la bei ya mafuta. “Tunaponunua mbuzi huko mikoani tunakutana na bei kubwa. Ukijumlisha gharama za usafiri na matunzo, inatulazimu kuuza kwa bei ya juu ili kuepuka hasara,” alisema muuzaji mwingine.

Baadhi ya wanunuzi waliokutwa sokoni hapo walikiri kuwa mwaka huu bei zimepanda ikilinganishwa na kipindi kama hiki mwaka jana, jambo lililowalazimu baadhi yao kuongeza bajeti au kutumia muda mrefu kutafuta mbuzi wenye bei nafuu.

“Mwaka jana nilinunua mbuzi kwa bei nafuu zaidi, lakini safari hii bei zimepanda sana. Kwa sasa mbuzi wanaanzia Sh 250,000 wakati mwaka jana walikuwa wanaanzia Sh 200,000, ingawa bado tunanunua kwa sababu ni sehemu ya maandalizi ya Eid,” alisema mmoja wa wanunuzi.

Licha ya changamoto hizo, wafanyabiashara wa soko hilo wameeleza matumaini yao kuwa biashara itaimarika zaidi kadri siku ya Sikukuu ya Eid al-Adha inavyokaribia kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya wanyama wa kuchinja. SOMA: Ruzuku ya chanjo, utambuzi kuwezesha biashara ya mifugo kimataifa

Katika mazingira yaliyojaa pilikapilika za biashara, sauti za mbuzi na majadiliano ya bei, Soko la Vingunguti linaendelea kuwa kitovu muhimu cha biashara ya mifugo kwa wakazi wa Dar es Salaam wanaojiandaa kuadhimisha moja ya sikukuu kubwa katika dini ya Kiislamu.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button