BENKI ya Dunia imeipongeza Tanzania kwa usimamizi mzuri wa uchumi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayopata fedha kutoka kwenye taasisi hiyo ikilinganishwa na nchi nyingine nyingi za Afrika.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayesimamia Kundi la Kwanza la Nchi za Kanda ya Afrika, Dk Floribert Ngaruko ametoa pongezi hizo alipokutana na kuzungumza na ujumbe wa Tanzania.
Ujumbe huo unaongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba kwenye mikutano ya Kipupwe ya Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) jijini Washington D.C nchini Marekani.
Dk Ngaruko alisema Tanzania ni nchi ya mfano katika usimamizi wa sera za uchumi na fedha na licha ya changamoto za Covid-19 na vita inayoendelea baina ya Urusi na Ukraine, tathmini ya benki hiyo inaonesha uchumi wa Tanzania uko imara ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika.
“Tanzania ni nchi ya kupigiwa mfano kwa usimamizi mahiri wa masuala ya uchumi mpana, si tu kwa nchi za Afrika Mashariki, bali kwa nchi za Afrika, ambapo kiwango cha ukuaji uchumi cha wastani wa asilimia 5.4 ni cha juu, na ninawapongeza sana,” alisema Ngaruko.
Aidha, alipongeza uhusiano kati ya Tanzania na Benki ya Dunia na kuahidi kuwa benki hiyo itaendelea kuisaidia Tanzania katika jitihada za kukuza uchumi na kuwaondolea umasikini wananchi wake.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu alisema uchumi wa Tanzania unazidi kuimarika, na serikali itaendelea kuchukua hatua kuhakikisha unazidi kukua.
Alisema katika kipindi cha robo tatu ya mwaka 2022/2023, uchumi umekua kwa asilimia 5.2 ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka wa fedha uliotangulia 2021/2022 na kutokana na mipango iliyowekwa utakua zaidi hadi kufikia wastani wa zaidi ya asilimia 6.3 miaka michache ijayo.
Aidha, aliishukuru Bodi ya Wakurugenzi ya benki hiyo kwa kuiidhinishia Tanzania Dola za Marekani bilioni 1.635 katika mzunguko wa 20 wa IDA (Julai 2022 – Juni 2025) za utekelezaji wa miradi sita ya maendeleo.
“Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi makini wa Mheshimiwa Dk Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania, tunaahidi kuwa tutasimamia na tutatumia fedha hizo kwa umakini ili kufikia malengo yaliyokusudiwa,” alisema Dk Mwigulu.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango Zanzibar, Dk Saada Mkuya Salum aliishukuru Benki ya Dunia kwa kusaidia ustawi na maendeleo ya Wazanzibari kwa kufadhili miradi ya kiuchumi na kijamii ikiwamo ya elimu na ujenzi wa miundombinu ya usafiri wa anga.
“Ujenzi wa miundombinu hiyo imekuza sekta ya utalii lakini bado tuna changamoto ya upatikanaji wa nishaji ya umeme wa uhakika na tunaamini tutaendelea kushirikiana na Benki yako kutatua changamoto hiyo na changamoto nyingine zinazotukabili,” alisema Dk Mkuya.
Mpaka sasa Benki ya Dunia imewekeza zaidi ya Dola za Marekani bilioni 7.2 sawa na takribani Sh trilioni 16.7 kwa ajili ya kutekeleza miradi zaidi ya 29 nchini Tanzania.
Kati ya miradi hiyo, 24 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 6.41 ni ya kitaifa na mingine mitano yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 0.75 ni ya kikanda.