Benki ya NMB yadhamini tena mkutano mkuu ALAT

BENKI ya NMB imechangia kiasi cha Sh milioni 120 kufanikisha maandalizi ya mkutano mkuu wa Jumuiya ya Tawala za Serikali za Mitaa (ALAT) wa mwaka huu unaonza leo jijini Mbeya.

Akikabidhi hundi ya mchango huo wa udhamini wa shughuli hiyo ya siku tatu, Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna, alisema wataendelea kushirikiana na ALAT kulihudumia taifa.

Mkutano huo wa 36 wa jumuiya hiyo unafanyika katika Hoteli ya Eden Highlands ambapo ndipo makabidhiano ya hundi ya kuufanikisha yalifanyika jana na kuhudhuriwa na uongozi wa juu wa taasisi hiyo na wafanyakazi wa NMB.

“Uhusiano kati yetu na ALAT ni wa muda mrefu na umekuwa wa manufaa makubwa kwa pande zote mbili. Kwa miaka mingi tumekuwa na mashirikiano na ALAT katika ngazi zote kuanzia halmashauri hadi ngazi ya taifa,”  alisema  Zaipuna kabla ya kukabidhi hundi hiyo.

“Katika kuendelea kuimarisha mahusiano yetu, kama benki tumeona ni vyema tushiriki katika kufanikisha mkutano huu utakaoanza kesho (leo) kwa kuchangia kiasi cha Sh milioni 120,” aliongeza.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi wa mkutano huo ambao kauli mbiu yake inasisitiza kuongeza tija katika ukusanyaji na matumizi ya mapato katika halmashauri kama msingi bora wa maendeleo endelevu ya wananchi.

Katibu mkuu wa ALAT, Elirehema Kaaya aliishukuru benki ya NMB kwa udhamini huo huku akisisitiza kuwa benki hiyo imekuwa sio tu mshiriki

mwema wa ALAT lakini kwa serikali kwa ujumla kwani wamekuwa wakishiriki katika shughuli nyingi za kiserikali na kuchangia shughuli za kimaendeleo hususani katika sekta ya elimu na afya.

Naye  Makamu Mwenyekiti wa ALAT taifa, Sima Constantine Sima aliipongeza benki ya NMB kwa udhamini huo na kuwasihi kuendelea kushirikiana vyema na ALAT kwa mustakabali wa maendeleo ya wananchi.

Mkutano Mkuu wa ALAT wa mwaka jana ambao pia mdhamini wake mkuu alikuwa ni Benki ya NMB ulifanyika Dodoma na kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 500 kutoka halmashauri 185 za majiji, wilaya na manispaa kote nchini.

 

 

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x