Benki ya Ushirika iwe mkombozi kwa ushirika

MOJA ya sekta ambazo katika siku za karibuni imekuwa ikipata mafanikio makubwa na kuonesha ufanisi ni sekta ya ushirika.
Sekta hii kwa muda mrefu ilikuwa imegubikwa na sintofahamu na kuhusishwa na mambo mengi yasiyovutia mbele ya jamii, yakiwamo ya unyonyaji wa wanachama wake pamoja na wizi uliogubika vyama vya ushirika na wakulima ambao ni sehemu kubwa ya wadau wa ushirika.
Lakini siku za karibuni, serikali kupitia Wizara ya Kilimo na kwa kutekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho kilichounda serikali, imefanya juhudi kubwa za kuhakikisha ushirika unakuwa kimbilio la wanachama wake na wadau wengine wanaohusika au kuunganishwa na wanaushirika.
Moja ya mafanikio ya ushirika ni kuzinduliwa kwa Benki ya Ushirika Tanzania mapema wiki hii mkoani Dodoma ambako yatakuwa makao makuu ya benki hiyo ambayo imeanzishwa kwa kuziunganisha Benki ya Ushirika ya Kilimanjaro (KCBL) na Benki ya Wananchi ya Tandahimba (TACOBA).
Uanzishwaji wa benki hii ulikuwa ni kilio cha muda mrefu cha wanaushirika, lakini changamoto kadhaa zilikwamisha hilo, ikiwamo suala la mtaji kama alivyoeleza Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa uzinduzi huo Jumatatu wiki hii.
Kwa sasa ndoto hiyo imetimia, na Benki ya Ushirika Tanzania imeshaanza kazi na ni tegemeo la wanaushirika wenyewe na taifa, kwa sababu hii ni nyenzo nyingine katika kuinua sekta ya ushirika na kilimo Tanzania.
Yapo manufaa mengi ya kuwa na benki hii yakiwamo ya kuongeza upelekaji wa mitaji kwa wakulima na sekta nzima ya kilimo, kuongeza tija kwenye kilimo na kuongeza mchango kwenye Pato la Taifa, na kuinua maisha ya wanaushirika.
Kwa hiyo, hakuna shaka kwamba benki hii itakuwa mkombozi kwa wakulima na wanaushirika nchini kwani watakuwa na mahali pa kukimbilia kupata mitaji ya kuendeshea shughuli zao kwa kupata mikopo kupitia benki yao.
Hili linathibitishwa na nguvu kubwa iliyoanza nayo benki hii kwa kuwa na mtaji wa Sh bilioni 58, matawi manne, mawakala 58 na maelfu ya wateja ambao kimsingi huu pia ni mtaji mkubwa na uthibitisho kuwa benki hii ilikuwa inasubiriwa kwa hamu.
Rai yetu kwa watendaji wa benki na watumishi wake kwa ujumla, wafanye kazi zao kwa uadilifu na uaminifu na kuifanya benki hii iwe mkombozi wa wanaushirika na ifanye kile ambacho serikali imekikusudia ilipoamua benki ianzishwe.
Haitakuwa jambo jema kama uadilifu na uaminifu utakosekana, jambo ambalo tunaamini halitakuwapo.
Tunataka kuona benki hii ikiwa ya mfano na kichocheo katika ukuaji wa sekta ya kilimo na ushirika zilizoko chini ya uongozi wa Rais Samia zimepata mafanikio makubwa na taifa linaona mchango mkubwa wa sekta hizi.
Ni vyema pia benki na Wizara ya Kilimo kwa ujumla kuzingatia maelekezo yote ya Rais Samia ikiwamo kuzingatia ubunifu, vyama vya ushirika kushirikiana na benki hiyo, kujenga ushirika imara, kutumia mifumo ya Tehama na kuhamasisha wakulima wajiunge kwenye ushirika ili kunufaika na fursa za mitaji na kujiimarisha kiuchumi.