Benki yajidhatiti huduma kidijitali

BENKI ya Absa Tanzania imesema imefanya uwekezaji mkubwa katika huduma zake za kibenki kwa njia za kidigitali ili kuunga mkono juhudi za serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha huduma za kibenki zinawafikia watanzania wengi na kwa gharama nafuu.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Kitengo cha Wateja Binafsi wa benki hiyo, Ndabu Lilian Swere wakati wa droo ya kwanza ya kampeni inayoendelea ya ‘Tumia Ushinde’ (Spend & Win), ambayo lengo lake kubwa ni kuhamasisha wateja wa benki hiyo na watanzania kufanya miamala mbalimbali ya kibenki kwa kutumia kadi ama huduma za kibenki kwa njia za kidigitali.

“Kampeni hii ya miezi mitatu ina lengo la kuwazawadia gari wateja wetu wanaofanya miamala ya kibenki kwa kutumia kadi za ATM ama huduma za kidigitali kwa kutumia mifumo yetu inayowawezesha wateja kupata huduma kiuharaka na kiurahisi hivyo kutimiza malengo yao.

Advertisement

“Sisi kama Absa Benki Tanzania tumeimarisha huduma zetu za kidigitali ili kwenda sambamba na jitihada zinazofanywa na serikali kusaidia kufikisha huduma za kibenki kwa wale ambao hawajafikiwa na huduma hizi huku wakiendelea kutumia mifumo ya kibenki ya kiasili.

“Mifumo ya kidigitali ya benki yetu ni ya haraka na tumeimarisha kwa kiwango cha kimataifa mifumo ya usalama hivyo tunapenda kuwatoa hofu wateja wetu wote kuendelea kufanya miamala kwa kutumia mifumo yetu ya kidigitali bila hofu yoyote”, amesema  Ndabu.

Naye Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Absa Tanzania, Aron Luhanga alisema kampeni hiyo inaenda sambamba na lengo kuu la kuwepo kwa benki hiyo ambalo ni kuiwezesha Afrika na Tanzania ya Kesho, hatua moja baada ya nyingine ikiwezeshwa na chapa mpya ya benki hiyo isemayo ‘Stori yako ni ya thamani’.

“Tunapotoa zawadi hii kwa wateja wetu na huku tukiboresha huduma zetu kwa njia za kidigitali tunaamini kuwa tunasaidia kuandika stori mbalimbali za washindi na wateja wetu, lakini pia tunaisaidia serikali yetu kuandika stori yake ya kuona huduma za kibenki zinawafikia watanzania wengi kila kona ya nchi yetu”, amesema Luhanga.