Bil 19.17/- kujenga stendi ya kisasa Geita

HALMASHAURI ya Manispaa ya Geita imesaini mkataba wenye thamani ya sh bilioni 19.17 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa kituo cha mabasi cha kisasa cha mkoa katika eneo la Magogo.

Fedha za mradi wa stendi mpya ni sehemu ya Mkopo wa Benki ya Dunia (WB) wenye lengo la kutekeleza Mradi wa Uboreshaji Miundombinu ya Miji Tanzania (TACTIC).

Mkataba wa kutekeleza mradi ni miezi 15 kuanzia Juni 15, 2025 hadi Septemba 14, 2026 chini ya mkandarasi M/s SIHOTECH Engeneering Company Ltd in JV pamoja na AMJ Global Multi Contractors.

Akizungumza katika hafla ya kusaini mkataba huo iliyofanyika mjini Geita, Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita, Yefred Myenzi amesema kituo hicho cha mabasi kitakuwa suluhisho la kituo cha mabasi cha sasa.

Amesema stendi mpya inajengwa katika eneo lenye ukubwa wa hekta 10.9 na itakuwa na uwezo wa maegesho ya mabasi 42, bajaji 100 na pikipiki 152 na kuchangia kiasi cha sh milioni 274.12 kwa mwaka.

“Tulikuwa tunaingiza takribani sh laki sita mpaka laki saba kwa siku, lakini kwa stendi mpya kutakuwa na ongezeko la magari pamoja na huduma nyingine na itawza kuingiza takribani sh milioni 1.2 kwa siku,” amesema Myenzi.

Mkandarasi wa kampuni ya SIHOTECH Engeneering, Mhandisi Adam Sebastian amesema tayari wamefanya maandalizi ya vitendea kazi na nguvu kazi ya kutosha kukamilisha mradi huo kwa wakati.

Mhandisi Adam amesema mradi huo unatarajia kuzalisha ajira zaidi ya 200 kuanzia hatua ya awali mpaka kukamilisha ili kufanikisha matakwa na hatua zote za utekelezaji wa mradi kwa ufanisi zaidi.

Meya wa Manispaa ya Geita, Costantine Morandi amesema mradi huo utawafuta machozi wananchi na viongozi wa manispaa ya Geita baada ya kilio cha muda mrefu kutokana na stendi isiyostahimili mvua.

Mwenyekiti wa Umoja wa wasafirishaji mkoa wa Geita, Esmail Hamis amesema stendi mpya ya mkoa wa Geita itavutia wawekezaji wengi zaidi wa sekta ya usafirishaji mkoani humo na kuongeza fursa za ajira.

Mkuu wa wilaya ya Geita, Hashimu Komba amemtaka mkandarasi kuheshimu matakwa ya mkataba ili kufanikisha azima ya serikali ya awamu ya sita kuboresha miundombinu ya kiuchumi na kijamii.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button