Bil 2.2/- zakusanywa makosa barabarani miezi mitatu Pwani

PWANI: JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani limekusanya Sh bilioni 2.2 kutokana na faini za papo kwa papo kutokana na makosa ya usalama barabarani katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita.
Aidha, madereva 38 walifungiwa leseni zao kwa makosa mbalimbali ya usalama barabarani.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Kibaha, Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, Salim Morcase alisema fedha hizo zilizotokana na faini walizopigwa madereva kwenye maeneo mbalimbali.
Morcase alisema kuwa waliweza kukamata makosa 74,446 ambayo yalifanywa na madereva na kupigwa faini za papo hapo katika kipindi hicho cha Septemba hadi Novemba mwaka huu.
“Katika kujenga uelewa juu ya elimu ya usalama barabarani wanafunzi 3,234 walipata elimu hiyo katika shule za msingi 42 na shule za sekondari 36 na vyuo vya udereva viwili,” alisema Morcase.
Alisema katika kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka wanawakumbusha wananchi wanaotarajia kusafiri kwenda mikoa mbalimbali kwa kutumia vyombo vya moto, kuzingatia sheria za usalama barabarani na madereva wazoefu ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika.
“Tunatoa rai kwa wananchi kuendelea kulinda amani na utulivu kwa kufuata sheria na kanuni za nchi ili kujiepusha na uvunjifu wa amani hapa nchini,” alisema Morcase.



