Bil 26/-kujenga MUHAS kampasi ya Kigoma

SHILINGI bilioni 26 zinatarajiwa kutumika katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Kampasi ya Kigoma ambapo tayari kampuni ya ujenzi ya China Jiangxi International and Technical Co. Ltd na chuo hicho wamesaini mkataba kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho.

Utiaji saini huo umefanyika eneo kitakapojengwa chuo hicho Eneo la Kisez Ujiji ambapo Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhambwa amewakilisha chuo hicho huku Peng Chao akiwakilisha kampuni hiyo iliyoshinda tenda ya ujenzi.

Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye pamoja na viongozi mbalimbali na wananchi wa mkoa wameshuhudia utiaji saini huo.

Mratibu wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET), Profesa Erasto Mbugi amesema ujenzi wa kampasi ya Kigoma unapaswa kukamilika Juni, 2026.

SOMA: Miradi 135 ya utafiti yafanyika MUHAS

Profesa Mbugi amesema ujenzi huo utahusisha jengo la utawala litakalotumiwa na watu 60, ukumbi wa mihadhara utakaochukua watu 150, maabara ya computer, maktaba, maabara sita za kufundishia, bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 111 na ukumbi wa mikutano wenye uwezo wa kuchukua watu 300,000 na uwanja wa michezo.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa MUHAS, Profesa Appolinary Kamuhabwa amesema wanafunzi 5900 wanatarajia kudahiliwa na chuo hicho kitakapokamilika na kwamba ujenzi wa kampasi hiyo ni mradi wa kimkakati wa serikali katika kupanua elimu ya juu katika sekta ya afya nchini.

Profesa Kamuhabwa amesema kampasi hiyo ya Kigoma itatoa fursa kubwa katika kutoa mafunzo na kufanya tafiti hasa eneo linalopakana na nchi za ukanda wa maziwa makuu.

Naye Mkuu wa mkoa Kigoma amesema ujenzi huo unatoa uhakikisho wa mkoa kukabiliana na upungufu wa wataalam katika sekta ya afya ambapo ujenzi wa chuo hicho chuo hicho na ujenzi wa hospitali ya rufaa ya kanda vitachangia kufanya miradi hiyo kuwa sehemu ya utalii wa tiba kwa wageni wa ndani na nje ya nchi.

Habari Zifananazo

Back to top button