Bil 50/- zafanikisha umilikishaji ardhi nchini

WAZIRI wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Angeline Mabula amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha wizara yake kupata Sh bilioni 50 kwa ajili ya programu ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi nchini.

Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango iliipatia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Sh bilioni 50 kwa ajili ya kuzikopesha halmashauri 55 kutekeleza Programu ya Kupanga, Kupima na Kumilikisha ardhi nchini.

Alisema utolewaji wa kiasi hicho cha fedha kumewezesha Mkoa wa Mwanza kupatiwa Sh bilioni 6.691 zilizosaidia kutekeleza miradi ya kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Dk Mabula alitoa shukrani hizo juzi jijini Mwanza mbele ya Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango wakati wa uzinduzi wa stendi mpya na ya kisasa ya mabasi na maegesho ya malori iliyopo eneo la  Nyamhongolo wilayani Ilemela.

Alisema uwezeshwaji wa fedha uliofanywa na serikali katika sekta ya ardhi umeisaidia halmashauri yake, Manispaa ya Ilemela kuwa na mradi wa kuuza viwanja alioueleza kuwa umeonesha mafanikio makubwa.

“Kuhusu masuala ya ardhi, namshukuru rais wetu Samia kwa kuipatia wizara shilingi bilioni 50 na kati ya kiasi hicho mkoa wetu wa Mwanza umepata shilingi bilioni 6.91, pesa ambazo zimeisaidia sana upimaji viwanja katika halmashauri zetu ikiwemo Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,” alisema.

 

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button