Bilionea Microsoft atembelea hifadhi Tanzania
MMOJA wa wanahisa wa kampuni mashuhuri duniani ya Microsoft na akihudumu kwa miaka 14 kama Mtendaji Mkuu wa Masuala ya Teknolojia katika kampuni hiyo, Dk Nathan Myhrvold amekamilisha mapumziko yake ya kiutalii nchini katika Hifadhi ya Taifa za Nyerere na Ruaha na kuondoka akiwa amefurahia kuwa nchini na familia yake.
Awali Dk Nathan akizungumza na ugeni wa watendaji wa Wizara ya Maliasili na Utalii ulioongozwa na Katibu Mkuu, Dk Hassan Abbasi, Mei 9, 2023 walipokuwa nchini Marekani aliahidi kuja Tanzania kupumzika na ametimiza ahadi hiyo.
“Ninavutiwa sana na vivutio vya utalii vya Tanzania. Nimeshafika Serengeti na Ngorongoro huko nyuma na safari hii nimebahatika kutembelea Ruaha na Nyerere haya ni miongoni mwa maeneo mazuri sana duniani. Tumefurahia sana,” alisema Nathan kabla ya kuondoka kwa ndege yake binafsi Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam jana kurejea Marekani.
“Ni faraja kwamba tulipokuwa Mei kule Seattle, Marekani na kupata fursa ya kukutana naye pamoja na mipango mingine aliyokuwa nayo alishawishika kuja Tanzania tena na tumemsikia hapa mwenyewe akisema amefurahia akiwa na familia yake na leo (jana) kwa niaba ya waziri wetu, Mohamed Mchengerwa, tumefika hapa kuwapa zawadi kidogo na kuwaaga,” alisema Dk Abbasi, akiwa na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Utalii (TTB), Damasi Mfugale.
Dk Nathan, pamoja na Microsoft na kampuni ya Intellectual Venture ambayo ni mwanzilishi na mtendaji mkuu, pia amewekeza pamoja na Bill Gates katika kampuni nyingine kubwa ya utafiti wa masuala ya umeme salama ya TerraPower.
Anatajwa kuwa mmoja wa wanasayansi na wagunduzi wakubwa wa nyakati hizi na mmoja wa wagunduzi wa programu ya “microsoft windows,” akiwa pia ni mwandishi mwenza na Bill Gates wa kitabu mashuhuri duniani kiitwacho “The Road Ahead.”
Kupitia taasisi yake ya Intellectual Ventures, Nathan anatajwa kuwa miongoni mwa Wamarekani watatu wakubwa wanaomiliki kisheria na kuzitumia kibiashara hakimiliki zenye thamani ya mabilioni ya gunduzi mbalimbali za kisayansi.
Dk Nathan ambaye kwa upande mwingine pia ni mtafiti wa sayansi za vyakula na amejenga maabara maalumu ya utafiti wa vyakula akiandika pia mfululizo wa vitabu vya: “Modernist Cuisines: The Art na Science of Cooking,” ameeleza kufurahishwa na ladha za baadhi ya vyakula alivyokula Tanzania kama ugali, mtori na supu ya mbuzi. Ameahidi kuendelea na tafiti za vyakula vya Tanzania.