Bilionea Mtanzania, Rais Ruto wajadili uwekezaji

KENYA: MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya Amson Group, Edha Nahdi amefanya mazungumzo na Rais wa Kenya, William Ruto kuhusu uwekezaji wa upanuzi wa kiwanda cha saruji cha Bamburi Cement kwa awamu ya pili wenye thamani ya Dola milioni 380 ambayo ni sawa na zaidi ya Sh bilioni 960.

Mazungumzo hayo yamefanyika katika Ikulu ya Nairobi na kuelezwa kuwa Nahdi mwenye umri wa miaka 37 pekee, amefanikisha ununuzi wa Kampuni ya Bamburi Cement kwa Dola milioni 182 sawa na Sh bilioni 500 na kuingia kwenye rekodi ya uwekezaji mkubwa zaidi kufanywa na Mtanzania nje ya nchi.

Kwa mujibu wa vyanzo vya kiuwekezaji, inaelezwa kuwa uwekezaji huu unazidi ule uliowahi kufanywa na mfanyabiashara, Rostam Aziz aliyekuwa amewekeza nchini Kenya kupitia kampuni yake ya Taifa Gas kwa Dola milioni 130 ambayo ni sawa Sh bilioni 338.

Mkataba wa ununuzi wa Bamburi Cement unatajwa kama uwekezaji mkubwa zaidi wa kibinafsi kutoka kwa kampuni ya Kitanzania nchini Kenya tangu kuvunjika kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki mwaka 1977.

Aidha, uwekezaji huo unaelezwa kuwa unaimarisha nafasi ya Amson Group kupanua shughuli zake katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Katika hatua nyingine, Amson Group imeonesha nia ya kuwekeza zaidi nchini Uganda, baada ya Bamburi Cement kukamilisha uuzaji wa hisa zake 70% katika kampuni tanzu ya Hima Cement kwa kampuni za Sarrai Group na Rwimi Holding, kwa thamani ya takribani dola milioni 84 ambayo ni sawa na Sh bilioni 214 mnamo Machi 2024.

Amson Group, inayomilikiwa na familia ya Nahdi, inafanya biashara katika nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Zambia, Malawi, Msumbiji, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Burundi, na sasa inatarajiwa kuwa mzalishaji mkubwa zaidi wa saruji katika Afrika Mashariki.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button