Bilioni 10.9 zatumika masomo udaktari bingwa
DAR ES SALAAM: Jumla ya Sh bilioni 10.9 zimetengwa ili kuwawezesha wanafunzi 1,109 kwenye masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi kusoma.
Ufadhili huo unatolewa kupitia Dk Samia Super-Specialized Scholarship Programme kwa masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi kwa mwaka wa masomo 2023/2024.
Waziri wa Afya,Ummy Mwalimu amesema hayo wakati akifungua mkutano wa Mwaka wa chama cha Madaktari bingwa wa magonjwa ya ndani Tanzania (APHYTA) uliofanyika Jijini Dar Es Salaam.
“Serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwa madaktari bingwa katika kuwaendeleza kitaaluma kupitia programu ambayo imetoa nafasi za ufadhili wa masomo ya ubingwa kwa mwaka wa masomo 2023/2024, kwa wanafunzi 1,109 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 582 ukilinganisha na mwaka wa masomo 2022/2023.” amesema Waziri Ummy.
Amesema, katika idadi ya wanafunzi wote ambao wamepata ufadhili kupitia programu hiyo, wanafunzi 79 watasomea udaktari bingwa wa magonjwa ya ndani na kati yao madaktari 11 sawa na asilimia 33 wamekwenda kusoma ubingwa bobezi wa magonjwa ya ndani.
Aidha, Waziri Ummy ametoa wito kwa madaktari vijana kujitokeza kwa wingi kwenda kujiendeleza katika masomo ya ubingwa bobezi hususan kwenye magonjwa ya ndani na wakirudi wakubali kupangiwa sehemu yoyote kwa kuwa mikoa mingine pia inahitaji madaktari bingwa bozezi.
“Kupitia muundo huu mpya wa Sekta ya Afya, tutaweza kuwatambua kwa kuwawekea mazingira mazuri madaktari wenye ubobezi katika maeneo mbalimbali ikiwemo wa masuala ya magonjwa ya ndani.” amesema Waziri Ummy
Katika hatua nyingine Waziri Ummy amewataka madaktari hao kujadiliana na kuja na mapendekezo ya jinsi ya kupunguza magonjwa yasiyoambukiza kwa kuwa kwa sasa kumekuana ongezeko kubwa la magonjwa hayo.
Pia, Waziri Ummy amewataka madaktari hao kujadiliana na kutoa maoni yao katika muongozo wa Kitaifa wa matibabu pamoja na orodha ya Taifa ya dawa ili kama kuna mapungufu yaweze kurekebishwa.