Bilioni 4/- zalipa walimu Geita

SERIKALI imeweka wazi kuwa ndani ya kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita jumla ya walimu 5,061 wa mkoa wa Geita wamelipwa madai yao yenye thamani ya Sh bilioni 4.6 ikiwemo malimbikizo ya mshahara
Aidha jumla ya Sh bilioni 2.2 zimelipwa kwa ajili ya uhamisho kwa walimu 1,028 wa mkoa wa Geita, huku walimu 1,839 wamepandishwa madaraja na walimu 876 wakibadilishiwa muundo wa utumishi mkoani hapa.

Naibu waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Dotto Biteko amesema hayo katika hafla ya katika kilele cha kliniki ya awamu ya nne ya Samia ya kutatua kero za walimu mkoani Geita.
Dk Biteko amesema pia serikali ilitumia sh milioni 368.8 kwa ajili ya walimu wote ambao wamepandishwa madaraja kwa mseleleko mkoani Geita
Ameongeza kuwa ndani ya kipindi cha miaka minne Sh bilioni 4.2 zimelipwa kama malipo ya likizo huku Sh milioni 25 zikilipwa kama malipo ya matibabu ya walimu Geita kwenye maeneo ambayo bima ya afya haifanyi kazi.
Amesema dhamira ya serikali ya awamu ya sita ni kumaliza kero za watumishi ikiwemo walimu ambapo aliwaagiza Wakurugenzi na wakuu wa Wilaya nchini kuanzisha utaratibu wa kukutana na walimu na kusikiliza kero zao.

Amesema timu ya Kliniki ya Samia ya kusikiliza na kutatua kero za walimu imebaini matatizo mengi yanayowakabili walimu ambayo yangeweza kutatuliwa kwenye halmashauri lakini hayajafanyiwa kazi.
“Taifa linalopiga hatua kwenye maendeleo usiache kuwekeza kwenye elimu na elimu kwenye utatu wake tuna mitaala, utahini na udhibiti ubora”, alisema na kuongeza;
“Kwenye mnyororo wote huo huwezi kufanikisha elimu kama huna mwalimu bora aliyemotishwa na anaependa kazi yake”amesema Dk Biteko.
Amesema kliniki hiyo inawakumbusha walimu kuwa wao ni nguzo muhimu ya Taifa na kuwataka walimu kutoa shida zao kwa haki na uwazi kwakuwa Serikali ndio yenye dhamana ya kusimamia maslahi ya wengi.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella amesema mbali na changamoto za utumishi kwa walimu pia zipo za kimfumo ambazo zimefanya walimu kuingia kwenye matatizo hasa na Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa.
“Mfumo wetu wa Nest unamasharti magumu walimu wamesomea ualimu sio uhasibu wanahitaji kujengewa uwezo maana wanapokosea kwenye mfumo wa manunuzi wanajikuta kwenye mikono ya Takukuru”amesema Shigella.
Makamu wa rais wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) Suleiman Komba ameiomba serikali kuunda chombo kimoja kinachoweza kushughulikia masuala ya ajira kwa walimu ili kuondoa changamoto zinazojitokeza mara kwa mara.
Mratibu wa kliniki ya Samia, Afredy Kusaga amesema takribani walimu 1,200 katika Wilaya za Bukombe, Chato na Geita wamefikiwa na huduma ya kliniki ya walimu ya Samia ya kutatua changamoto zinazowakabili.



