Binti darasa la nne adaiwa kujinyonga

JESHI la Polisi linachunguza kifo cha mwanafunzi wa darasa la nne Shule ya Msingi Kambarage wilayani Kibaha mkoani Pwani, Tatu John ambaye alikutwa amejinyonga kwa kutumia kamba ya chandarua kwenye chumba cha kulala nyumbani kwao.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo alithibitisha kutokea tukio hilo eneo la Mtaa wa Mkoani B.
Kamanda Lutumo aliwaeleza waandishi wa habari jana kuwa tukio hilo lilitokea Februari 19 saa 9 alasiri ambapo familia hiyo ilihojiwa na Jeshi hilo kuhusiana na tukio hilo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa Mkoani B, Shabani Kasamya alisema alipokea simu kutoka kwa mjumbe wa mtaa wake akimueleza kuwa kuna mtoto amejinyonga ndani ya nyumba.
Kasamya alisema kuwa kabla hajaenda kwenye nyumba palipotokea msiba, alitoa taarifa polisi ili wafike kwenye eneo la tukio.
“Nilipofika nyumbani niliwakuta wafiwa wapo na mjumbe ndipo walipoingia ndani ulipo mwili wa marehemu na kumkuta akiwa ameingiza kichwa ndani ya kamba ya chandarua ambayo imefungwa dirishani mkono wa kulia na kushoto,” alisema Kasamya.
Alisema tukio hilo lilifanyika kwenye dirisha la chumba ambacho walikuwa wanalala watoto na walimkuta marehemu amepiga magoti na polisi walifika wakapiga picha na kuchukua vipimo kisha wakaondoka na mwili kuupeleka Hospitali ya Tumbi.