NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amehimiza nchi za Afrika zitumie vyanzo vyake kuzalisha umeme.
Dk Biteko amesema hayo New Delhi, India ameposhiriki katika mjadala wa mawaziri wa sekta ya nishati kutoka India, Qatar, Uingereza na Tanzania.
Mawaziri hao walijadili mada iliyohusu mpango mpya wa dunia wa biashara ya nishati.
Alitoa mfano kuwa Tanzania ina madini ya makaa ya mawe ya kutosha na urani ambayo yanafaa kuzalisha umeme.
Alisema, hata hivyo kumekuwa na changamoto ya kupata ufadhili wa kuyaendeleza kwa ajili ya kuzalisha umeme
kwa vile yanatajwa kusababisha uchafuzi wa mazingira.
Alisema makaa ya mawe yanaweza kutumika kuzalisha umeme kwa kutumia teknolojia ya kisasa yenye kuondoa
sumu ya kaboni.
Dk Biteko alisema takribani watu milioni 600 Afrika hawajafikiwa na huduma ya umeme, hivyo kwa kuzalisha
umeme kwa kutumia vyanzo mbalimbali, ikiwemo makaa ya mawe itawezesha lengo la kufikishia umeme watu hao
kwa haraka.
“Afrika inachangia uchafuzi wa mazingira kwa kiasi kidogo kwa sababu ni bara masikini lakini inatajwa kuwa na mchango sawa na mataifa mengine, mabadiliko ya matumizi ya nishati hayakwepeki, nchi ziruhusiwe kuwa na uendelezaji endelevu wa rasilimali zake kwa ajili ya kuwa na usalama wa nishati,” alisema.
Aliongeza, “lazima tuangalie ukweli na hali halisi, mfano Qatar au India hali yao ya upatikanaji umeme ni tofauti na Tanzania, hatutaweza kutumia njia ya aina moja kwa ajili ya kutatua changamoto za masuala ya umeme kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea ni lazima kutumia njia tofauti.”
Dk Biteko alisema Tanzania ina umeme wa kutosha na ziada ya megawati 750. Imejenga miundombinu ya kusafirisha na kuunganisha umeme na nchi jirani kama vile Kenya, Burundi na Rwanda ili kuwezesha biashara ya umeme.
Waziri anayeshughulikia masuala ya nishati kutoka Uingereza, Ed Milliband ameipongeza Tanzania kwa
mafanikio katika uzalishaji na usambazaji umeme kwa wananchi.