NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema Serikali ya Tanzania imejizatiti kuboresha na kuimarisha sekta ya kilimo kwa kuja na mipango kadhaa yenye lengo la kuongeza fursa kwa wakulima nchini.
Dk Biteko ameyasema hayo jijini Delhi, India wakati akishiriki mkutano kuhusu masuala ya mazao jamii ya mikunde.
“Tunaongeza uwekezaji katika utafiti na kuboresha upatikanaji wa teknolojia za kisasa za kilimo ambapo kila ofisa ugani nchini amepewa vifaa vyote muhimu ikiwemo pikipiki na kompyuta ili kutoa huduma nzuri na kwa wakati kwa wakulima wetu,” amesema.
Amesema serikali pia imeboresha shughuli za usafirishaji wa bidhaa ikiwa ni pamoja na kurahisisha michakato ya
uuzaji mazao.
“Tanzania inaendeleza ujenzi wa reli ya kisasa (SGR) ambayo itaimarisha usafirishaji wa bidhaa yenye urefu wa takribani kilometa 500 kutoka Bandari ya Dar es Salaam hadi Dodoma ambayo imekamilika na inatumika,” amesema.
Vilevile, amesema kupitia mradi wa BBT serikali imewezesha vijana kwa kuwapa ardhi, fedha na upatikanaji wa masoko sambamba na kuongeza huduma za kifedha za kidijiti.
“India ni soko muhimu kwa mazao ya jamii ya kunde kutoka Tanzania na tunaweza kupata mafanikio makubwa zaidi. Leo nawaalika wawekezaji kutoka India na nchi nyingine duniani kuja kuwekeza katika sekta ya kilimo ya Tanzania kuanzia uzalishaji wa kisasa wa soya hadi uwekezaji katika mifumo ya usimamizi wa mavuno,” amesema.
Akizungumzia maendeleo ya sekta ya mazao jamii ya mikunde, amesema kuwa 2023, Tanzania ilizalisha tani
250,000 za mbaazi ikiwa ni ongezeko la asilimia 56 ikilinganishwa na mwaka 2018.
Inakadiriwa ifikapo 2030, Tanzania itakuwa na ukuaji mkubwa katika Pato la Taifa kupitia kilimo. Mauzo ya maharage mekundu yanatarajiwa kufikia Dola za Marekani bilioni 1.47, mbaazi (milioni 84) na choroko (milioni 115).
Aidha, ili kufikia uwezo huo, Tanzania imeweka mikakati ya kukuza sekta ya mazao jamii ya kunde kupitia Mfumo wa Stakabadhi Ghalani kwa wakulima kusajiliwa, kuboresha mbinu za kilimo na teknolojia, kuhakikisha ubora na viwango vya mazao kulingana na mahitaji ya soko.
“Mazao jamii ya kunde nchini Tanzania yanauzwa kupitia mnada wa mtandaoni ambao unatoa fursa kwa wafanyabiashara kupata taarifa kuhusu mizigo iliyohifadhiwa katika ghala lililosajiliwa,” alieleza.
Alisisitiza kuwa mfumo huo unahakikisha uwazi, ufuatiliaji na ufanisi katika biashara ya kimataifa.
Amesema mwaka jana pekee, kupitia mfumo huo, wakulima wa Tanzania walipata zaidi ya Dola milioni 91.31 kutoka katika biashara ya mbaazi, dengu na maharage ya soya.
Kutokana na hali hiyo, kiwango cha biashara kati ya nchi hizo mbili kimeongezeka na kufikia Dola bilioni 7.9 kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Pia, 2023 mauzo ya mbaazi kutoka Tanzania kwenda India yalifikia tani 186,447 yenye thamani ya Dola milioni 139.1.