Biteko azindua Zahanati ya Bungoni

DAR ES SALAAM: Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko Desemba 29, 2023 amezindua Zahanati ya Bungoni iliyopo mtaa wa Mafuriko Ilala jijini Dar es Salaam na kuwataka wananchi kutumia fursa ya uwepo wa huduma ya zahanati hiyo kutumia huduma badala ya kwenda mbali kufuata huduma za afya, kwani ni dhamira ya Serikali kusogeza huduma kwa wananchi.

“Niwaombe viongozi wenzangu tuliopewa dhamana na Rais kuhakikisha tunawahudumia kwa vitendo wananchi na kuinua hali za wanyonge kwa kuwapatia huduma bora wanazostahili.

” Amesisitiza Dk Biteko

Ujenzi wa zahanati hiyo ulianza mwezi Februari mwaka huu, kwa jitihada za wananchi na baadae Serikali na umegharimu kiasi cha Sh milioni 351, ukihusisha gharama za ujenzi, samani, dawa na vifaa tiba na umefadhiliwa na African Relief Agency na Taasisi ya Rahma International kutoka Kuwait na inamilikiwa kwa asilimia mia moja na Serikali.

Zahanati hiyo itakuwa na uwezo wa kuhudumia kata nne zilizopo Wilaya ya Ilala ambazo ni Ilala, Buguruni, Sharifu Shamba, na Mchikichini wapatao Elfu 12.

Akizungungumza wakati wa hafla hiyo, Mbunge wa Jimbo la Ilala na Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Azan Zungu amewataka watendaji kuhakikisha wanatumia vyema fursa za wafadhili wanaokuja kuwekeza Kwenye sekta ya afya na kuondoa mikwamo inayoweza kuchelewesha maendeleo.

Awali, akitoa taarifa ya mafanikio ya Idara ya Afya kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Jiji Dk, Zaituni Hamza amesema kuwa, wamefanikiwa kujenga jumla ya vituo vipya saba vya kutolea huduma na kupandisha hadhi zahanati tano kuwa vituo vya afya, hivyo kufanya jumla ya vituo vya afya kuwa 12.

Habari Zifananazo

Back to top button