DAR ES SALAAM: NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema kuwa, uwekezaji wowote unaofanywa katika Sekta ya Elimu lazima umguse Mwalimu kwani ndiye injini na kiongozi wa rasilimali zote zinazowekwa kwenye mfumo wa elimu nchini.
Kazi nzuri ya Walimu hapa nchini, imefanya ufaulu wa wanafunzi kutoka Shule ya Msingi kwenda Sekondari kuongezeka kutoka 907,802 mwaka 2021 hadi 1,092,984 mwaka 2023 ikiwa ni ongezeko la asilimia 20.4.
Dk Biteko amesema hayo leo alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika hafla ya kuzindua Programu ya Kuboresha Kada ya Ualimu nchini (GPETSP) katika Ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam hafla ambayo ilienda pamoja na kaulimbiu ya Walimu Wetu Fahari yetu.
“Mwalimu ndiye rasilimali kuu inayofanya rasilimali nyingine ziweze kuleta matokeo chanya kwenye Sekta ya Elimu, ndio maana mtaona programu tunayoizindua leo inaonesha kwa vitendo kuwa Serikali tunatambua kwamba lazima tuwekeze zaidi kwa Walimu kwenye mazingira ya kujifunza na ufundishaji lakini pia kuwatambua Walimu kuwa ninyi ndio watu tunaowategemea kufanya elimu yetu iweze kwenda mbele,” amesema Dk Biteko
Amesema, Rais Samia anafanya kila jitihada ili masuala yote yanayowahusu Walimu yafanyiwe kazi kwa kasi ikiwemo kuwapunguzia changamoto zinawazowakabili ili Walimu hao wajikite katika kusomesha na kutatua changamoto za watoto mashuleni.