BMT kuzifanyia tathimini kamati za mikoa 12

DAR ES SALAAM. BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) linategemea katika robo ya tatu ya mwaka huu wa fedha kutembelea Kamati za Michezo za mikoa 12, ili kutathimini utendaji kazi wa kamati hizo na kuhakikisha kamati hizo zimeundwa na zinatekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kanuni za taasisi hiyo
Kamati za Michezo za Mikoa hujumuisha Ofisa Tawala wa Mkoa husika, Ofisa Michezo Mkoa, wajumbe saba walioteuliwa na Mkuu wa Mkoa husika, mjumbe mmoja kutoka kila chama au shirikisho kilichosajiliwa katika mkoa huo pamoja na maofisa Tawala wa Wilaya na maofisa michezo wote walioko katika wilaya za mkoa husika.
Mkuu wa Kitengo cha Uendelezaji Michezo wa BMT, Benson Chacha amesema Kamati za Michezo za Mikoa ndizo zenye jukumu la kutekeleza majukumu ya BMT katika ngazi hizo ikiwamo usajili, kusimamia, kuendeleza vipaji, miundombinu, kuratibu mashindano n.k
Aesema kamati zitakazotembelewa ni za Mikoa ya Kagera, Shinyanga, Simiyu, Mara, Mwanza, Geita, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Singida na Tabora.
Pia amesema kuwa tathimini hiyo inalenga kuona utayari wa Kamati hizo jinsi zilivyojipanga kuendeleza sekta ya michezo katika maeneo yao ili kongeza ajira, kuimarisha amani na mshikamano, kuhamasisha jamii kushiriki michezo, kuleta watu pamoja na kufikia matarajio ya Dira ya Taifa ya 2050.
Amesema, tathimini hiyo itaangalia namna ambavyo kamati hizo zimechukua hatua madhubuti za kuimarisha utawala bora, uwazi na uwajibikaji katika kusimamia shughuli za vyama na mashirikisho ya michezo kwenye mikoa husika ili viweze kuendeshwa kwa kuzingatia misingi ya kitaifa ya uendeshaji wa michezo hiyo nchini.



