BARAZA la Michezo la Taifa (BMT) limewataka waandaaji wa mapambano ya ngumi za kulipwa nchini (promota) kufuata kanuni na taratibu za Kamisheni ya mchezo huo (TPBRC) ili kuepuka kusababisha sintofahamu kwa wadau wa michezo.
Hayo yamekuja baada ya baraza hilo kutangaza kuifungia taasisi inayojihusisha na ngumi, Goldenboy Boxing Promotion na kiongozi wake mkuu, Shomari Kimbau kutojihusisha na shughuli hizo kwa miaka miwili.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa wa Uhusiano na Mawasiliano wa BMT, Najaha Bakari alisema wamechukua uamuzi huo baada ya mwandaaji huyo kusababisha kutofanyika kwa pambano la Hassan Mwakinyo dhidi ya Patrick Allotey wa Ghana lililokuwa limepangwa kufanyika Mei 31, mwaka huu mkoani Dar es Salaam.
“Baraza limeamua kuchukua uamuzi huo baada ya Shomari Kimbau kushindwa kufuata na kuzingatia taratibu za Kamisheni ya Ngumi za Kulipwa (TPBRC), kitendo ambacho kinarudisha nyuma michezo pamoja na kuchafua taifa,” alisema Najaha.
SOMA: Mangungu: Mo ni jasiri
Alisema hawakuridhishwa na maelezo aliyoyatoa kupitia barua yake ya Juni 4, mwaka huu iliyomtaka atoe sababu zilizosababisha kutofanyika kwa pambano hilo na kudai hakuwa makini katika maandalizi yake.
Alisema BMT haitakuwa na huruma na mtu yeyote atakayefanya kitendo kama hicho kwa kumchukulia hatua kali za kinidhamu ili iwe fundisho