MKUU wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa ameiomba Kampuni ya simu ya Vodacom kuboresha huduma zake, ikiwemo kutumia muda mfupi kuhudumia wateja wanaotaka ufafanuzi wa huduma mbalimbali za kimtandao, ikiwemo utalii mbugani.
Ametoa kauli hiyo leo wakati akizindua duka jipya lililopo Aim Mall jijini Arusha sanjari na kukabidhi hundi ya Sh milioni 5.5 kwa mshindi wa bahati nasibu ya Tusua Mapene.
Akizungumza katika uzinduzi huo Mtahengerwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa katika filamu ya Royal Tour, ambayo imeongeza idadi ya watalii, hivyo kusababisha shughuli za utalii kukua, ikiwemo huduma za mawasiliano hasa vijijini.
“Hivi sasa watalii ni wengi, nawaomba Vodacom mboreshe huduma zenu za mawasiliano, lakini pia boresheni kitengo cha huduma kwa wateja kwa kuwahudumia muda mfupi,” amesema.
Awali Mkuu wa Vodacom Kanda ya Kaskazini , George Venanty amesema kampuni hiyo imekuwa mstari wa mbele kusogeza huduma kwa wateja na kwamba Arusha wana maduka zaidi ya 66, lakini pia wateja wanaojiunga na kampeni ya Tusua Mapene wanapewa zawadi mbalimbali.
Ametoa rai kwa wateja wa Vodacom waendelee kushiriki katika bahati nasibu zilizopo, ili wajishindie zawadi mbalimbali.