BoT kuhifadhi dhahabu tani 6 za tril 1.04/-

DODOMA – SERIKALI imesema ina lengo la kununua tani sita za dhahabu yenye thamani ya dola za Marekani milioni 400 sawa na zaidi ya Sh trilioni 1.045 za Tanzania.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba alisema hayo bungeni Dodoma juzi wakati akiwasilisha mapendekezo ya serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2024/25. Serikali imewasilisha bajeti ya Sh trilioni 49.35.

Dk Mwigulu alisema serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeanzisha utaratibu wa kununua dhahabu kwa ajili ya akiba ya taifa kwa lengo la kuimarisha akiba ya fedha za kigeni na kusaidia katika utekelezaji wa Sera ya Fedha. Alisema hadi Aprili mwaka huu, BoT ilikuwa imenunua dhahabu yenye thamani ya dola za Marekani milioni 26.

Dk Mwigulu alisema katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita kumekuwa na mafanikio katika sekta ya madini ikiwamo kuendelea kuongezeka kwa mchango wa sekta ya madini kwenye Pato la Taifa kutoka asilimia 7.3 mwaka 2021 hadi asilimia 9.0 mwaka jana.

SOMA: Wasomi, wanasiasa wakoshwa bajeti 2024/25

Alitaja mafanikio mengine ni kuongezeka kwa vituo vya ununuzi wa madini kutoka 61 mwaka 2020/21 hadi vituo 100 mwaka 2023/24 na kuanzishwa kwa soko jipya la madini hivyo kufikia masoko 42.

“Aidha, serikali imenunua mitambo mitano ya uchorongaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo inayotumika katika maeneo mbalimbali nchini,” alieleza Dk Mwigulu.

Alisema serikali inaendelea kuhamasisha viwanda vya ndani vya kuchenjua dhahabu kufanya taratibu za kupata Ithibati ya London Bullion Market Association (LBMA) ili kuwezesha dhahabu inayosafishwa kutambuliwa kwenye masoko ya kimataifa na kununuliwa kwa ajili ya kuhifadhiwa kama fedha.

Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo aliwaeleza wabunge kuwa mwaka jana thamani ya mauzo ya madini nje ya nchi ilikuwa dola za Marekani bilioni 3.55 ikilinganishwa na dola za Marekani bilioni 3.39 mwaka 2022 sawa na ongezeko la asilimia 4.6.

Habari Zifananazo

Back to top button