BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imesema uchumi wa nchi umetulia.
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba ameeleza kuwa katika nusu ya kwanza ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 sekta ya fedha iliendelea kuwa thabiti ikiwa na viwango vya chini vya vihatarishi.
Tutuba ameeleza hayo katika taarifa ya Mapitio ya Nusu Mwaka ya Tamko la Sera ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha
2024/2025.
Amesema uchumi wa Tanzania Bara unatarajiwa kuendelea kukua kwa kasi na Pato la Taifa (GDP) linatarajiwa kukua kwa takribani asilimia sita katika nusu ya pili ya mwaka 2024/2025.
Ukuaji huo unatarajiwa kuchangiwa na hali nzuri ya hewa, upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na uwekezaji
unaoendelea kufanyika katika miundombinu ya umwagiliaji.
Sekta ya ujenzi inatarajiwa kuendelea kushamiri kutokana na uwekezaji kwenye miradi mikubwa ya miundombinu ikiwamo Reli ya Kisasa ya Umeme (SGR), barabara, madaraja na viwanja vya ndege.
SOMA: Uchumi wa Tanzania kupaa kwa 6% mwaka 2025
Pia, huduma za usafirishaji, uwepo wa umeme wa uhakika na utekelezaji wa sera madhubuti ya fedha na ya bajeti vinatarajia kuchangia ukuaji huo.
“Kwa upande wa Zanzibar, uchumi unatarajiwa kukua kwa zaidi ya asilimia sita, ukichangiwa na shughuli za utalii, ujenzi na upangaji wa majengo,” ameeleza Tutuba.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa mfumuko wa bei unatarajiwa kuendelea kuwa tulivu katika nusu ya pili ya mwaka
2024/2025 ukikadiriwa kuwa takribani asilimia tatu kwa Tanzania Bara na chini ya asilimia tano kwa Zanzibar.
Tutuba ameeleza kuwa katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024/2025 mapato ya ndani yaliendana na malengo yakichangiwa na kuimarika kwa shughuli za uchumi na maboresho katika usimamizi na ukusanyaji wa kodi.
“Kwa upande wa Zanzibar utekelezaji wa bajeti ulikuwa wa kiwango cha juu, ambapo mapato ya serikali yalivuka lengo kwa asilimia 4.8. Mapato ya kodi yalivuka lengo kwa asilimia 3.6, kutokana na maboresho katika usimamizi wa kodi pamoja na utayari wa wananchi kulipa kodi kwa hiari. Kwa serikali zote, matumizi yaliendelea kufanyika kwa kuzingatia upatikanaji wa mapato,” alieleza.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa sekta ya benki iliendelea kuwa na ukwasi na mtaji wa kutosha, na kutengeneza faida.
“Rasilimali za benki ziliongezeka sambamba na amana zikichochewa na ongezeko la huduma za uwakala wa benki, pamoja ongezeko la matumizi ya mifumo ya kidijiti katika utoaji wa huduma za kibenki,” alisema Tutuba.
Ameongeza: “Ukwasi katika benki uliendelea kuwa wa kutosha na mikopo chechefu ilipungua hadi kufikia asilimia
3.3 mwishoni mwa mwezi Desemba 2024 kutoka asilimia 4.1 mwishoni mwa mwezi Juni 2024”.
Kwa mujibu wa Tutuba, mifumo ya malipo iliendelea kufanya kazi kwa ufanisi na BoT iliendelea kuboresha mifumo kwa lengo la kuongeza ufanisi na upatikanaji wake.
Aidha, alieleza kuwa BoT iliendelea kuchukua hatua za kuongeza matumizi ya kidijiti katika kufanya miamala nchini badala ya kutumia fedha taslimu.
Tutuba alieleza kuwa sekta ya nje iliendelea kuimarika katika nusu ya kwanza ya mwaka 2024/2025, sanjari na mwenendo wa uchumi wa dunia na wa nchini.
Alieleza kuwa urari wa malipo ya kawaida unakadiriwa kuwa na nakisi ya Dola za Marekani milioni 785.3 takribani nusu ya nakisi iliyorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2023/2024.
“Hali hii ilitokana na kuimarika kwa shughuli za utalii na ongezeko la mauzo ya dhahabu, korosho na tumbaku nje ya nchi,” alieleza Tutuba.
Aliongeza, “Urari wa malipo ya kawaida kwa upande wa Zanzibar ulikuwa na ziada ya dola za Marekani milioni 321.5, ikilinganishwa na ziada ya dola za Marekani milioni 219.2, kutokana na ongezeko la mapato yatokanayo na shughuli za utalii”.
Tutuba alieleza kuwa katika robo ya pili ya Mwaka wa Fedha 2024/2025 ukwasi wa fedha za kigeni uliongezeka kwa kiasi kikubwa.
“Ongezeko hili lilitokana na kuimarika kwa mazingira ya kiuchumi duniani hususani kushuka kwa viwango vya riba ya sera ya fedha katika nchi zilizoendelea kiuchumi na kupungua kwa bei za mafuta ghafi,” alisema gavana.
Aliongeza: “Aidha, mapato ya fedha za kigeni kutokana na shughuli za utalii, mauzo ya dhahabu, korosho, na
tumbaku yalichangia.