BoT yaja na mifumo kudhibiti mikopo kausha damu

SERIKALI imezindua mifumo miwili ya kidijiti ili pamoja na mambo mengine kunusuru Watanzania na mikopo umiza inayotolewa na riba kubwa.
Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema hayo Dodoma akizindua mifumo miwili ya kidijiti ya kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha zinazotolewa na taasisi zinazosimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na mazingira ya majaribio ya teknolojia ya huduma za fedha zinazodhibitiwa na BoT.
Dk Mwigulu alisema mageuzi yanayofanywa na serikali kwenye mifumo rasmi ya kifedha yanalenga kuwanusuru Watanzania kwenye wimbi la mikopo umiza au kausha damu inayotolewa kwa riba kubwa.
“Watu wanaokwepa urasmi ndio wanaoingia kwenye mikopo ambayo wanakopa Shilingi milioni tatu wanatakiwa kurudisha ndani ya miezi mitatu na wanarudisha mara tatu, utaratibu wa kukwepa urasmi ndio unaowaingiza kwenye matatizo,” alisema Dk Mwigulu.
Aliongeza: “Lakini ukienda kwenye taasisi ya fedha iliyo rasmi unachukua hiyo Shilingi milioni moja na kutakiwa kurejesha baada ya miaka miwili au zaidi na sio kwenda kuchukua kwenye mikopo umiza inayokutaka kurejesha ndani ya miezi mitatu kwa riba kubwa”.
Alisema anaamini mfumo huo utakuwa suluhisho la malalamiko yakiwamo mikopo umiza na itaongeza imani kwa umma kutumia huduma rasmi za fedha na kuboresha uwajibikaji kwa watoa huduma za fedha.
Alisema kichocheo cha kukua kwa huduma za fedha ni kutokana na teknolojia ya fedha ambayo imerahisisha wananchi kutuma na kupokea fedha.
Dk Mwigulu alisema Watanzania wanaotumia huduma rasmi za fedha imeongezeka na kufikia asilimia 76 kwa mwaka 2023 kutoka asilimia 57 mwaka 2013.
Alisema kasi ya Watanzania kutumia huduma rasmi za fedha inaridhisha na ifikapo mwaka 2028, Tanzania itafikia asilimia 85 ya watumiaji wa huduma jumuishi za fedha.
“Teknolojia ya huduma za fedha imerahisisha sana, watu wanaachana na tabia ya kutembea na fedha taslimu. Nitoe rai kwa Watanzania tusiogope mageuzi haya, tutakapofikia kila huduma kulipia kielektroniki itarahisisha sana ukuaji wa uchumi wetu na mazingira ya biashara,”alieleza Dk Mwigulu.
Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba alisema pamoja na juhudi za kuongeza upatikanaji wa huduma jumuishi za kifedha nchini, bado kuna changamoto zikiwamo kutokuwa na mazingira rafiki kwa ukuaji wa teknolojia na ubunifu katika mifumo ya utoaji wa huduma rasmi za fedha.
Aliitaja changamoto nyingine ni kuwapo kwa idadi kubwa ya watoa huduma wasiokuwa rasmi, kiwango cha chini cha elimu ya fedha kwa watumiaji, uhusiano hafifu baina ya watoaji na watumiaji wa huduma rasmi za kifedha na mfumo analojia.
Alisema BoT kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Watumiaji Jumuishi wa Huduma za Fedha wamechukua hatua zilizowezesha kuzinduliwa kwa mifumo hiyo.
Alisema mifumo hiyo inalenga kuboresha utoaji wa huduma za kifedha na kukuza matumizi ya teknolojia ya fedha na kumlinda mtumiaji wa huduma rasmi za fedha.
Awali, Naibu Gavana wa BoT, Sauda Msemo alisema mfumo wa kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma za fedha utaongeza ufanisi na uwazi katika kushughulikia malalamiko ya watumiaji wa huduma hizo ili kuongeza imani.