Boti ya mizigo yateketea moto, yajeruhi 2 Kigoma

KIGOMA; WATU wawili wamejeruhiwa kwa moto baada ya boti ya mizigo inayojulikama kwa jina la Mv Suala la Muda kuteketea kwa moto usiku wa kuamkia  jana Bandari ndogo ya Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji, mkoani Kigoma.

Mmiliki wa Boti hiyo, Hussein Kakozi akizungumza na waandishi wa habari bandarini hapo baada ya tukio hilo, alisema boti yake ilikuwa imeegeshwa katika bandari hiyo ikitarajia kuondoka alfajiri ya Januari 15, 2026 kuelekea Jamhuri ya Kidemokrasi ya  Congo (DRC), ikiwa na mizigo mbalimbali.

Kamanda wa Polisi Mkoa Kigoma, Filemon Makungu  akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, alisema watu wawili wamejeruhiwa katika ajali hiyo, ambao ni mabaharia wa boti Chakuvuta Mashaka na Jerome Ally, waliokuwa wanajaribu kufanya uokoaji na wamelazwa Hospitali ya Mkoa Kigoma Maweni.

Boti za mizigo na abiria zikiwa zimeegeshwa katika bandari ndogo ya Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji

Hata hivyo Kamanda Makungu hakubainisha mizigo iliyokuwa imebebwa kwenye boti hiyo na thamani yake na kwamba uchunguzi unaendelea.

Mmoja wa mashuhuda waliokuwepo wakati ajali hiyo inatokea, Ramadhani Shabn Mkazi wa Kibirizi Manispaa ya Kigoma Ujiji alisema kuwa awali walisikia mlipuko ukitokea ndani ya boti hiyo uliofuatiwa na moto baadaye wakasikia kelele za watu kuomba msaada.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Kigoma Maweni, Dk Lameck  Mdengo amethibitisha kupokewa kwa watu wawili waliojeruhiwa kwenye ajali hiyo ya boti, ambapo Jerome aliruhusiwa kurudi nyumbani baada ya matibabu na Mashaka anendelea na matibabu.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button