Bunge laidhinisha bajeti Wizara ya Fedha

DODOMA; BUNGE limeidhinisha bajeti ya Wizara ya Fedha yenye makadirio ya zaidi ya Sh trilioni 20 kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Mapema asubuhi leo Juni 4, 2025, Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba, aliwasilisha bungeni mapitio ya utekelezaji wa mpango na bajeti kwa mwaka 2024/25 na mapendekezo ya mpango na bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2025/26.
“Kwa mwaka 2025/26, mafungu nane (8) ya Wizara ya Fedha yanaomba kuidhinishiwa matumizi ya jumla ya shilingi trilioni 20.19 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo.
“Kati ya kiasi hicho, shilingi trilioni 19.43 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida ikijumuisha mishahara shilingi trilioni 1.10, matumizi mengineyo shilingi trilioni 18.33 na matumizi ya maendeleo shilingi bilioni 757.79.
“Aidha, ninaomba Fungu 045 – Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi kuidhinishiwa jumla ya shilingi bilioni 122.52 kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo.
“Kati ya kiasi hicho, shilingi bilioni 110.42 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 12.10 matumizi ya maendeleo,” amesema Waziri Nchemba.