Bunge laitaka kahawa stakabadhi ghalani

BUNGE limeazimia serikali ijumuishe mazao ambayo bado hayajaingizwa kwenye mfumo wa stakabadhi za ghala ikiwemo kahawa.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Deodatus Mwanyika amesema hayo bungeni Dodoma wakati akiwasilisha taarifa ya mwaka ya shughuli za kamati hiyo kwa mwaka 2024.

Mwanyika amesema pia Bunge limeazimia serikali iweke mfumo mzuri wa uendeshaji na usimamizi wa maghala ili kudhibiti tabia za wamiliki wa maghala kuwalipisha wakulima gharama zisizowahusu.

Advertisement

Ametaja azimio lingine ni serikali iongeze kasi ya kushirikiana na sekta binafsi kujenga maghala ya kutosha katika maeneo ya wakulima.

Mwanyika amesema pia Bunge limeazimia serikali itoe elimu kwa wakulima kuhusu umuhimu wa kuuza mazao yao kwa kutumia mfumo wa stakabadhi za ghala.

Amesema changamoto ya uchache wa maghala na baadhi kuwa mbali na maeneo ya mashamba hulazimisha wakulima kusafiri umbali mrefu kupeleka mazao.

Amewaeleza wabunge kuwa changamoto hiyo husababisha wakulima waingie gharama kubwa kusafirisha mazao umbali mrefu.

Kwa mujibu wa Mwanyika pia madalali hutumia fursa hiyo kununua mazao kutokakwa wakulima kwa bei ndogo na hivyo kukwamisha utekelezaji wa mfumo wa stakabadhi za ghala.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *