WADAU wa sheria wakiwamo wanasheria na mawakili wamelishauri Bunge lirekebishe sheria inayompa mamlaka Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kuzuia dhamana za washitakiwa.
Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Pauline Gekul alisema bungeni Dodoma kuwa dhamana katika kesi za jinai ni haki iliyowekewa utaratibu wa kisheria.
Gekul alisema kwa mujibu wa sheria za Tanzania, kuna makosa yanayodhaminika na yapo makosa ambayo hayana dhamana, na Kifungu cha 148 (5) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai Sura 20 kimeainisha makosa yote ambayo hayana dhamana.
“Hivyo kwa makosa yote ambayo hayajatajwa na kifungo hicho yana dhamana ambayo ni haki ya mshitakiwa,” Gekul aliwaeleza wabunge.
Wakili Francis Stola amedai kuwa dhamana ni haki ya kila mshitakiwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kwamba kabla ya washitakiwa kutiwa hatiani wanakuwa hawana hatia mpaka mahakama itakapothibitisha.
Stola alisema dhamana inastahili kutawaliwa na dhana kwamba mtu anapotuhumiwa na kushitakiwa anadhaniwa kuwa hana hatia mpaka shauri litakaposikilizwa na mahakama na iseme kama ana hatia au hana.
Alisema Kifungu 147 (a) cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinasema mahakama ndiyo yenye mamlaka ya mwisho katika utoaji haki za watu nchini hivyo waruhusu mahakama ifanye kazi yake na si DPP.
“Msingi wa pili ni uhuru wa mahakama kuamua kwani ndiyo iliyopewa mamlaka ya kuhakikisha haki inatendeka katika mfumo wa haki jinai. Dhana hizi mbili zimekuwa zikimomonyolewa,” alisema Stola.
Aliongeza: “Sheria iiachie mahakama mamlaka yake ya kuzuia au kutoa dhamana ikiangalia mazingira yake na hata kama DPP atawasilisha maombi ya kuzuia dhamana, mahakama iamue ili kuepuka watu wasio waaminifu kuzuia dhamana za washitakiwa kwa sababu zao.”
Wakili Sadock Magai alishauri Kifungu namba 148 (4) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinachokataza dhamana kiondolewe na mahakama iachiwe mamlaka ya kuzuia dhamana.
Magai alidai kitendo cha DPP kuzuia dhamana ni kinyume cha Kifungu namba 13 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambacho kinaeleza mtuhumiwa hapaswi kuwekwa rumande bila kusikilizwa au kuhukumiwa na mahakama.
“Mahakama ndiyo iwe na mamlaka ya mwisho nani apewe na nani asipewe dhamana na DPP abaki na mamlaka ya kuhisi kuwa mtu ana kosa, kumkamata, kumpeleleza na kumfikisha mahakamani, asipewe mamlaka ya kuzuia mtu dhamana,” alisema Magai.
Alisema Kifungu namba 13 (6) (b) cha Katiba ya Tanzania kinaeleza kuwa ni marufuku kwa mtu anayeshitakiwa kwa kosa la jinai kuchukuliwa kama mtu mwenye kosa hilo mpaka itakapothibitika kuwa ana hatia ya kutenda kosa hilo. Wakili Peter Madeleka alisema haki ya dhamana kwa mshitakiwa inapatikana kwa mujibu wa Ibara ya 13 (6) (d) ya Katiba ambayo inatamka kuwa mtu yeyote si mkosaji hadi atakapotiwa hatiani na mahakama. Madeleka alisema mtuhumiwa au mshitakiwa anatakiwa afurahie haki ya kuwa huru kama inavyoelekezwa na ibara ya 15(1) ya Katiba ya Tanzania.
“Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) Kifungu cha 148(5) kimeweka orodha ya makosa ambayo mtuhumiwa akikabiliwa nayo moja kwa moja hayana dhamana kitendo kinachopingana na Katiba,” alisema Madeleka.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema haki ya dhamana ni miongoni mwa haki za binadamu kama ilivyoainishwa katika Ibara ya 13(6) (b) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Henga alisema haki hiyo imezuiwa na Kifungu cha 36 cha Sheria ya Uhujumu Uchumi na Uhalifu wa Kupangwa Sura namba 200 na Kifungu cha 19 cha Sheria ya Usalama wa Taifa ambayo inampa mamlaka DPP kuzuia dhamana kwa yeyote aliyetuhumiwa kutenda kosa chini ya sheria hizo.
“Mamlaka ya DPP chini ya sheria hizo hayawezi kuzuiwa na mahakama yoyote. Hivyo, Kituo cha Sheria na Haki za binadamu kinapendekeza kurekebishwa kwa sheria hizo ili kutoa mamlaka yasiyokuwa na udhibiti wa mahakama ili kumpa mtuhumiwa haki chini ya ibara 13 (6) (b),” alisema Henga