Bunge latabiri uchumi kukua kwa asilimia 6

BUNGE limesema uchumi unatarajiwa kukua kwa asilimia 6.0 mwaka huu na asilimia 6.1 mwaka 2026.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti, Oran Njeza amesema hayo bungeni Dodoma akiwasilisha taarifa ya kamati hiyo tangu Februari, mwaka jana hadi Januari mwaka huu.

Njeza amesema mwaka 2025 uchumi unatarajia kukua kufikia asilimia 5.4. Wakati akihutubia taifa kuuaga mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2025 Rais Samia Sukuhu Hassan amesema mwaka jana uchumi wa nchi uliendelea kuimrika.

Advertisement

“Uchumi wa nchi yetu uliendelea kuimarika na kuwanufaisha wananchi, kati ya mwezi Januari hadi Juni 2024
uchumi ulikuwa kwa asilimia 5.4 ikilinganishwa na asilimia 4.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2023,” amesema Rais Samia.

Njeza amesema ili malengo ya kukuza uchumi yafikiwe ni vyema serikali iendelee kutekeleza miradi ya maendeleo na kuimarisha uhusiano wake na washirika wa maendeleo ili kuendelea kupata fedha za kutekeleza miradi nchini; na
aliwaeleza wabunge kuwa ili mfumko wa bei uendelee kubaki katika wigo wa asilimia tatu hadi nane, kamati
inaishauri serikali iendelee kuhakikisha kuna chakula cha kutosha ili kuzuia mfumko wa bei unaoweza kusababishwana ukosefu wa chakula.

“Kufuatia ufanisi kwenye ukusanyaji wa mapato katika kipindi cha nusu mwaka, utekelezaji wa bajeti ya serikali unatarajiwa kufikia malengo yaliyokusudiwa,” amesema Njeza.

Kuhusu makusanyo, Njeza alisema katika kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu, serikali inatarajia kukusanya Sh trilioni 24.56 kutoka vyanzo vyote ikijumuisha mapendekezo ya nyongeza ya bajeti ya Sh bilioni 845.7 na kutumia kiasi hicho katika utekelezaji wa shughuli za serikali.

Amesema kamati inaishauri serikali iendelee kusimamia matumizi sahihi ya mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji
wa mapato, mifumo ya ununuzi na kuhimiza nidhamu ya matumizi sanjari na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima ya fedha za umma.

Aidha, Njeza amesema Bunge limeazimia serikali ifanye tathmini ya misamaha yote ya kodi ili kuhakikisha kwamba misamaha inayotolewa ina tija na inakuwa ndani ya kiwango kinachokubalika cha chini ya asilimia 1.3 ya Pato la Taifa.

Amesema kiwango cha utoaji wa misamaha ya kodi kinatakiwa kutozidi asilimia 1.3 ya Pato la Taifa kwa mwaka 2024.

Njeza alisema pia Bunge limeazimia serikali ihakikishe kiwango cha mapato cha asilimia 20 cha kodi ya majengo kinarejeshwa katika halmashauri kwa wakati, pamoja na kuangalia uwezekano wa kuongeza kiwango hicho.

Amesema pia limeazimia katika mwaka wa fedha 2024/2025 serikali iongeze kiwango kinachorejeshwa kutokana na kodi ya majengo kutoka asilimia 20 ya sasa hadi walau asilimia 50 kwa kipindi cha usajili wa majengo ili kuharakisha utambuzi na uthamini wa majengo pamoja na kuandaa rejesta na kisha kurudisha asilimia 20 ya awali.

Njeza alisema pia limeazimia serikali iboreshe mfumo wa Tausi ili kuwezesha ukusanyaji wa kodi ya majengo
ikiwamo usimikaji wa Moduli ya Kodi ya Majengo katika mfumo wa Tausi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa 137 na iajiri wataalamu wa kutosha katika halmashauri kwa ajili ya kufanya kazi ya uthamini wa majengo.

Alisema pia Bunge limeazimia serikali ifanye marejeo ya kina ya matumizi ya serikali na kupunguza matumizi yasiyo ya lazima kabla ya kuanza utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano unaotarajiwa kuanza mwaka 2025/2026 hadi 2030/2031.

Kamati hiyo imeishauri serikali ihakikishe sera na sheria za kiuchumi ni thabiti, wazi, na zinazochochea uwekezaji na upunguze urasimu na uweke mazingira wezeshi ya kufanya biashara na uwekezaji ili kuvutia uwekezaji mpya.

Pia, imeishauri serikali iunde na kuimarisha mikataba ya biashara na ushirikiano wa kiuchumi na nchi na mashirika  mbalimbali duniani na ianzishe na balozi katika nchi ambazo ni washirika wakubwa wa kibiashara ili kukuza
biashara na uwekezaji.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *