PWANI: MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Umeme (TANESCO) Gissima Nyamo-Hanga amesema kwa sasa jumla ya mashine tano zimekamilika kwa asilimia 100 yaani mashine namba 9, 8, 7, 6 na 5 na tayari zimeanza uzalishaji wa umeme katika Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) lililopo mkoani Pwani.
Gissima Hanga amesema hayo leo Desemba 20 katika ziara ya uongozi wa shirika hilo ulipotembelea mradi huo kujionea kasi ya maendeleo ya ujenzi na kuweka mkazo kwa wasimamizi kuhakikisha usimikaji wa mashine nne zilizobakia unafanyika ipasavyo ili umeme utakapozalishwa uingizwe kwenye Gridi ya Taifa.
” Tumetembelea mradi huu kujionea shughuli zinazoendelea na kuweka msisitizo wa usimamizi bora kwa maeneo ambayo bado hayajakamilika ambapo utekelezaji kwa ujumla umefikia asilimia 99.55 huku shughuli za uzalishaji wa umeme zikiwa zimeanza na wastani wa megawati 1175 zinazozalishwa kutoka mashine tano za mradi huu zimeingizwa kwenye Gridi ya Taifa,” amesema Gissima.
Amebainisha kuwa utekelezaji wa usimikaji wa mashine namba nne umefikia asilimia 100 ambapo kwa sasa mashine hiyo ipo kwenye majaribio huku mashine namba tatu ikiwa kwenye asilimia zaidi ya 87 za usimikwaji, asilimia ambazo zinadhihirisha kuwa kiwango cha utendaji kazi ni kizuri.
Amewahimiza wasimamizi wa mradi kuhakikisha wanaendeleza bidii kusimamia maeneo ambayo bado hayajakamilika kuhakikisha kazi inafanyika kwa viwango vilivyoainishwa wakati wa usanifu wa mradi huo.
“Niwaombe msimamie vizuri kuhakikisha ufanyaji kazi wa mashine unakuwa ni mzuri ili umeme unaoendelea kuzalishwa unapoungwa kwenye Gridi ya Taifa usilete changamoto yoyote,” amesisitiza Gissima.
Katika hatua nyingine, Gissima ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa pamoja na Wizara ya Nishati na viongozi wake wote kwa namna ambavyo mara zote imeunga mkono kwa kutoa fedha na ushirikiano katika kusimamia utekelezaji wa mradi mpaka kufikia hatua iliyopo sasa pamoja na miradi mingine mingi inayoendelea nchini .
“Ninawaahidi watanzania wenzangu kuwa, sisi kama viongozi wa TANESCO tutahakikisha tunasimamia mradi huu kwa dhati na umadhubuti mkubwa ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kuleta tija ya kiuchumi na kijamii katika taifa letu la Tanzania,” alihitimisha Gissima.