CAG ataja mashirika yenye mitaji hasi  

CAG Charles Kichere

RIPOTI ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22 katika eneo la utendaji wa kifedha wa mashirika na taasisi imebaini mashirika 10 yenye mtaji hasi.

CAG ameeleza kuwa mashirika na taasisi hizo wana malimbikizo ya muda mrefu ya hasara na mikopo ili kujiendesha.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo kati ya mashirika hayo, matano ni ya kibiashara na manne si ya kibiashara.

Advertisement

Katika ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni na CAG hivi karibuni, Charles Kichere anayataja mashirika hayo kuwa ni Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL), kampuni ya Stamigold, kampuni ya Uchapishaji ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Benki ya TIB, kituo cha Kompyuta Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kampuni ya Chuo cha Teknolojia Dar es Salaam.

Mashirika mengine ni Mfuko wa Maendeleo ya Zao la Pamba, Bodi ya Pareto Tanzania, Bodi ya Maziwa Tanzania na Bodi ya Katani Tanzania.

“Kwa mfano, Mfuko wa Maendeleo ya Pamba uliripoti ongezeko la asilimia 525 katika malimbikizo ya hasara kutoka Sh bilioni 3.70 katika mwaka wa fedha 2020/21 hadi Sh bilioni 23.10 katika mwaka wa fedha wa 2021/22, hasa kutokana na kuongezeka kwa gharama za uendeshaji na kiasi cha madeni yasiyokusanyika,” alisema Kichere.

Alisema katika kampuni ya madini ya Stamigold ilikuwa na malimbikizo ya hasara yanayofikia Sh bilioni 58.44 hadi kufikia Juni 30, mwaka jana iliyopunguza mtaji wa kampuni. Hasara hiyo ilisababishwa na kupungua kwa uzalishaji wa madini kutokana na upungufu wa vifaa vya uchimbaji kutoka kwa mkandarasi.

Kichere alisema kuwa na mtaji hasi kunatia shaka ikiwa taasisi hizo zitaweza kudumu kwenye utoaji wa huduma na kutekeleza majukumu ipasavyo katika siku zijazo.

Alipendekeza mashirika na taasisi zingine za umma zifanye uchambuzi kuhusu hali yao ya kifedha, kutambua sababu za mtaji hasi na kuandaa mpango wa kushughulikia sababu za kuwa na mtaji hasi.

“Hii inaweza kujumuisha hatua za kupunguza gharama, kuboresha ufanisi, kuongeza mapato, kurekebisha madeni, kuweka mazingira rafiki ya ulipaji au kuuza mali zisizo za muhimu,” alieleza.

Aidha, alishauri mashirika au taasisi zingine ziombe msaada wa serikali ili kuongeza mtaji au kuwekeza katika biashara mpya ili kuwa na mapato ya kutosha kulipa madeni na kukuza mitaji ya taasisi.