–
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG ), CPA Charles Kichere amesema katika ukaguzi wake amebaini kuna dawa zenye thamani ya shilingi bilioni 8.16 zilizoagizwa na Halmashauri 10 kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD) hazikufikishwa kwenye vituo vya afya.
Akizungumza leo Aprili 6, 2023 CAG Kichere amesema pia alibaini Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) ulikataa madai ya ya shilingi bilioni 1.77 kutoka kwa Halmashauri 66 kwa sababu ya kutozingatia miongozo ya NHIF.
Amesema, pia amebaini miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 82.95 ya vituo vya afya katika Halmashauri 91 haijakamilika
Vilevile miradi yenye thamani ya shilingi bilioni 2.64 ambayo haijaanza huku miradi iliyokamilika katika Halmashauri 16 yenye thamani ya shilingi bilioni 4.93 haikuwa imeanza kutumika.
Kutokana na hali hiyo, amebaini pia kuna ongezeko la idadi ya vifo vya wajawazito zaidi ya wastani wa vifo 102 hadi 989 kwa kila vizazi hai 100,000 juu ya shabaha ya vifo 100 kwa kila vizazi hai 100,000 kwa Halmashauri 20 kwa mwaka 2021/22.
“Nilibaini kuwa, kwa miaka ya fedha 2020/21 na 2021/22, kulikuwa na vifo vya watoto wachanga 6,335 katika Halmashauri 20; hata hivyo, uwiano wa vizazi hai na vifo kwa watoto wachanga havikuweza kutambuliwa kwa vile takwimu za uzazi hazikupatikana.”Amesema
Aidha, amesema pia alibaini katika Halmashauri mbili kwamba kiwango cha vifo vya watoto wachanga kilikuwa juu sana ambapo ni Halmashauri ya Jiji la Mbeya ilikuwa na kiwango cha vifo 135 kwa kila vizazi 1000, huku Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya ikiwa na kiwango cha vifo 49 kwa kila vizazi 1000.
“Viwango hivi ni vya juu kuliko shabaha inayotarajiwa ya vifo 30 kwa kila watoto 1000 wanaozaliwa, ambavyo vinahitaji kufikiwa ndani ya mpango wa miaka mitano.”Amesema.