CBK: Acheni kutumia noti kwa mapambo

BENKI Kuu ya Kenya (CBK) imewaonya wafanyabiashara wa maua na wamiliki wa maduka ya zawadi dhidi ya kutumia noti kutengeneza shada la maua na mapambo mengine, ikisema tabia hiyo inaharibu fedha na kuathiri mzunguko wake.

Katika notisi ya umma iliyotolewa mwanzoni mwa Februari, CBK ilisema imebaini kuongezeka kwa matumizi ya noti kwa madhumuni ya mapambo, ikiwemo shada la pesa na maonyesho mbalimbali, hali inayokiuka matumizi sahihi ya fedha.

Onyo hilo limekuja baada ya kusambaa kwa video kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha noti zikikunjwa na kuunganishwa kwa ajili ya mapambo kwa kuzingatia rangi na thamani tofauti. CBK imesema matumizi hayo huharibu noti na kuzifanya zisiweze kutumika tena katika mzunguko wa fedha.

Aidha, benki hiyo imeeleza kuwa tabia hiyo huathiri utendaji wa mashine za kushughulikia fedha ikiwemo ATM, mashine za kuhesabu pesa na za kuchambua noti, hali inayosababisha fedha kukataliwa na kuleta gharama zisizo za lazima kwa benki na wananchi.

Hata hivyo, CBK imesisitiza kuwa haina pingamizi juu ya utoaji wa pesa taslimu kama zawadi, mradi noti hizo zisikunjwe, kubandikwa au kuharibiwa kwa namna yoyote. “Fedha inapaswa kubaki katika hali inayoruhusu mzunguko huru na kutekeleza jukumu lake kama chombo cha kubadilishana na hifadhi ya thamani,” ilisema CBK.

Benki hiyo imeonya kuwa mtu yeyote atakayebainika kuharibu noti anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kifungo cha hadi miaka saba jela. SOMA: Uchumi wa Kenya umeshuka 5.0% hadi 4.7%

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button