CCM Iringa wamtwisha mzigo Asas

HALMASHAURI Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), wilaya ya Iringa imemshtaki Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Bashir Muhoja kwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Salim Asas, ikidai hakuna uhusiano mzuri baina yao, hivyo kuathiri ufuatiliaji wa  utekelezaji wa Ilani yao.

Taarifa ya kikao hicho kilichohudhuriwa na wajumbe zaidi ya 130 na kutolewa na Mwenyekiti wake, Costantino Kiwele imemuomba MNEC huyo kuwasilisha malalamiko yao kwa Rais, Dk Samia Suluhu Hassan kuhusu hali inayoendelea wilayani humo ambayo  haina afya nzuri katika utekelezaji wa Ilani.

Akipokea malalamiko hayo Asas ameahidi kuyafikisha katika kikao cha Kamati ya Siasa ya Mkoa, ambayo moja ya wajumbe wake ni Mkuu wa Mkoa wa Iringa, ili yafanyiwe kazi kabla ya kufikishwa mamlaka za juu zaidi.

Asas alikumbusha umuhimu wa watendaji wa serikali kushirikiana na chama hicho, akisema wakati fulani makosa yao ya kiutendaji yamekuwa  yakikisababishia chama chao lawama kubwa kutoka kwa wananchi na washindani wao wa kisiasa.

“Yaani unaweza kuta kosa linafanywa na Mkurugenzi au mtendaji fulani lakini lawama zinakuja kwetu kwa sababu sisi ndio tumeunda hii serikali. Na badala ya watendaji hao kushukuru wakati fulani kwa kuwatetea, malipo yake ni kutotaka kushirikiana na sisi,” alisema.

Wakati huo huo, Asas ameitaka halmashauri hiyo kushirikiana na wana CCM wenzao kuhakikisha wanafanya kazi itakayokibakisha chama chao madarakani, kuendelea kukiimarisha chama hicho na kuisemea serikali kwa kazi zote inazofanya.

Pia ameahidi kuipa CCM wilaya hiyo msaada wa kifedha, ili iweze kukamilisha mradi wake wa ujenzi wa milango ya biashara pembezoni mwa ofisi zake itakayokuwa moja ya vyanzo vyake vya mapato.

Katika kujiimarisha zaidi kiuchumi ameshauri chama hicho katika ngazi mbalimbali kujikita katika kilimo cha miti na parachichi akisema, sekta hiyo inaweza kuzalisha mapato ya uhakika kama ikisimamiwa ipasavyo.

 

Habari Zifananazo

Back to top button