CCM Iringa yakaribisha maelekezo ya Kheri James

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa Iringa, Daudi Yasin amesema chama chao kinatambua uwezo binafsi wa kisiasa wa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Kheri James hivyo kipo tayari kupokea maelekezo yake kuelekea chaguzi kuu mbili za kiserikali zinazokuja.

Akitoa salamu za chama hicho katika hafla ya kumuapisha Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Joachim Nyingo, Yasin alisema; “Usiogope, njoo hata kwangu na utupe maelekezo maadamu tu yawe yale yatakayotupa njia itakayotupa ushindi.”

Yasin alisema akili, nguvu na macho yao kwasasa yemeelekezwa na chama hicho katika uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwakani.

“Na katika kufikia malengo yetu hatutakuwa na msalia mtume na mtumishi yoyote wa umma atakayekwamisha juhudi za Rais Dk Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi,” alisema.

Alimkumbusha Mkuu wa Mkoa, wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri zote za mkoa wa Iringa kutekeleza agizo la Rais linalowataka kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi.

“Sisi kama chama tutaendelea kuwa nyuma yenu. Tutatumia macho matatu kusimamia utekelezaji wa Ilani yetu ili kama tulivyoahidi ijibu changamoto za wananchi na yule atakayetukwamisha tutashughulika naye,” Yasin alisema katika hafla hiyo iliyohudhuriwa na watumishi mbalimbali wa serikali.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba alisema anatambua mwaka huu na mwakani kutakuwa na chaguzi na akaahidi uongozi wake kufanya kazi usiku na mchana kuupeleka mkoo huo mbele zaidi.

Akipongeza miaka mitatu ya Rais Samia, Serukamba alisema utawala wa mkuu huyo wa nchi umefanikiwa kutekeleza asilimia zaidi ya 80 ya ahadi zilizotolewa katika Ilani ya CCM jambo linalowapa kazi ndogo ya kumalizia palipo baki.

“Katika kipindi cha miaka mitatu ya Dk Samia kazi iliyofanyika ni ya kimapinduzi katika sekta zote, ikiwemo ya usafirishaji na miundombinu yake, umeme, maji, elimu, afya, kilimo, viwanda, uwekezaji na demokrasia-Rais amefanya mambo makubwa sana, tunaweza kusema kuliko hata mtangulizi wake,” alisema.

Aliwaomba watu wa CCM kutoa ushirikiano ili kazi ya kuwahudumia wananchi wa mkoa wa Iringa iwe rahisi na yenye mafanikio yatakayokiwezesha chama kupigiwa kura za kishindo katika chaguzi hizo zijazo.

“Tushirikiane kumlipa Rais deni lake. Deni hilo ni kumpa kura za heshima katika chaguzi zinazokuja. Awamu ya kwanza ni uchaguzi wa serikali za motaa na awamu ya pili ya deni hilo ni Uchaguzi Mkuu,” alisema.

Kuhusu kusikiliza na kutatua kero za wananchi, Serukamba aliahidi yeye na wasaidizi wake katika wilaya zote za mkoa huo kuanza shughuli hiyo mara baada ya mfungo wa Ramadhani.

“Tukimaliza mfungo wa Ramadhani tutapita kijiji kwa kijiji, mtaa kwa mtaa tukatoe elimu ikiwemo ya kipambana na udumavu lakini pia tutahakikisha tunapambana na uharifu wa aina zote ili kuufanya mkoa wetu kuwa mahali salama pa kuishi na kufanya maendeleo, ” alisema huku akiahidi kuhimiza ukusanyaji wa mapato ya serikali.

“Nawakaribisha pia wananchi kwa ushauri. Mnapokuja mje na mambo ya kujenga sio majungu; wakati wa kusemasema watu umepitwa-tujifunze kuvimiliana. Kuna wakati tunafanya kazi na tuanaowapenda na tusiowapenda, lazima tukubali hayo mazingira,” alisema.

Mkuu wa Wilaya ya Kilolo kwa upande wake alimshukuru Rais kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kuwatumikia wananchi wa wilaya hiyo akiahidi kwamba hatamuangusha.

“Naahidi kushirikiana na wananchi wote wa wilaya ya Kilolo kusukuma zaidi gurudumu la maendeleo ya wilaya, mkoa na Taifa kwa ujumla,” Nyingo alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button