CCM: Tukiheshimu sheria, hakuna machafuko

DAR-ES-SALAAM : CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria na taratibu za uchaguzi ili kuhakikisha mchakato wa uchaguzi mkuu unakuwa huru, wa haki na wenye kuzingatia amani na utulivu.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Zanzibar, Khamis Mbeto Khamis, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
“Endapo sheria zitazingatiwa kikamilifu, hakutakuwa na sababu ya machafuko. Amani na utulivu ni matokeo ya kuheshimu taratibu zilizowekwa kisheria,” alisema Khamis. SOMA: Uchaguzi Mkuu Oktoba 29
Amesisitiza kuwa ni wajibu wa vyama vyote vya siasa, pamoja na wadau wengine wa uchaguzi, kuhakikisha wanaheshimu sheria za uchaguzi ili kulinda mshikamano wa kitaifa na kuimarisha demokrasia nchini.
Aidha, Khamis ameonya dhidi ya jaribio lolote la kuingilia au kuhujumu kazi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), akibainisha kuwa hatua hizo zinaweza kuhatarisha ustawi wa maendeleo ya kijamii , kisiasa kwa Taifa.
Kauli hiyo imekuja wakati Tanzania ikijiandaa kuelekea uchaguzi mkuu ujao, ambapo wito umetolewa kwa wananchi, vyama vya siasa na taasisi mbalimbali kuhakikisha mazingira ya uchaguzi yanabaki kuwa ya amani, heshima na kufuata misingi ya kisheria.



