CCM yapawa neno watumishi wa serikali

SHINYANGA: CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kama kuna mtumishi wa serikali anaona hawezi kuwajibika aache kazi na kuwapisha wanaoweza kuwajibika wafanye kazi.
Katibu NEC, Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM Taifa, Kenani Kihongosi alieleza hayo akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara katika Kata ya Nyasubi Kahama Mjini mkoani Shinyanga ikiwa ni mwanzo wa ziara yake Kanda ya Ziwa.

Awali, Kihongosi alianza kwa kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi wa Kahama wakati akijibu kero hizo aliwataka watumishi kutimiza wajibu wao bila kusubiri viongozi wa chama kutoka taifani ndipo wazitatue.
Akieleza hayo Kihongosi alisema ni wazi kwamba kumekuwa na uzembe ambao umekuwa ukifanyika, akisitiza viongozi na watumishi waumma wote waliopewa dhamana wawajibike ipasavyo.
“Naomba sana kwa heshima kubwa kabisa na kwa unyenyekevu mkubwa sana kila aliyepewa dhamana na serikali ya chama hiki akatimize wajibu, kila ambaye analipwa mshahara, kodi za watendaji, akatimize wajibu,” amesema Kihongosi.

Ameongeza; “Na kero nyingine sio mpaka mtu atoke taifani aje atatue kero ndani ya nyanja ya mtu mwingine, na utaratibu ni rahisi, ukiona kazi ngumu acha wafanye wengine. Sio kila mtu ana mpango tumepanga, tunafuatilia, tumepokea, nimechukua nita”.

Kihongosi alieleza hayo baada ya kero iliyowasilishwa na wananchi wa eneo hilo waliyodai kuwa mkandarasi alipewa barabara ya Kahama Mjini lakini aliishia kuitindua na kuiacha ikiwa katika hali mbaya.



