Chalamila ataka barabara Ubungo-Kimara ikamilike haraka

MKUU wa Mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila amemtaka mkandarasi anayejenga barabara ya Morogoro kipande cha Ubungo -Kimara kukuongeza kasi ya ujenzi ili kupunguza msongamano wa magari.
Chalamila alitoa wito huo Aprili 10,2025 ikiwa ni siku ya pili ya ziara ya kukagua hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi Wilaya ya Ubungo na kutoa maagizo kwa viongozi wa halmashauri pamoja na wakandarasi kuhakikisha kuwa miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
“Haiwezekani kutoka pale ubungo mpaka Kimara utumie saa nne wakati kila siku tunavutia biashara masaa 24 na hiyo itakuwa siyo ufanisi wa kazi hivyo naomba ninyi Wakala wa Barabara nchini (TANROAD) na wakandarasi kufahamu umuhimu wa barabara hii kwani inatumika na magari mengi kwenda mikoa yote,”amesema Chalamila.

Ameongeza,”Endapo mtafanya kazi kwa uzembe tutasukumana sana,najua kuna barabara kimekamilika na hazina mabasi lakini serikali inafanya kila jitihada kuhakikisha mabasi yanapatikana na watoahuduma wataongezeka katika hali ya kawaida haiwezekani kufikiria kupaua nyumba ili hali ujamaliza kujenga nyumba,”
Amesema serikali haijalala bali inafanyia kazi changamoto za kisheria,kisera na nyingine ilikuhakikisha maendeleo yanafikiwa kwa wakati.
Mhandisi kutoka TANROADS, Beatrice Rweyemamu amesema mradi huo umegharimu kiasi cha Sh bilioni 83 na hadi sasa mkandarasi amekwisha lipwa Sh bilioni 21 huku kazi ikiendelea.

“Ni kweli kazi unaendelea lakini changamoto kubwa tunayokutana nayo ni msongamano wa magari hasa kunapotoa ajali,mvua kuonyesha na magari kuzima katika ya barabara na tunajitahidi kuzitatua kwa wakati na kuukamilisha kama linavyotarajiwa Aprili 30,mwaka huu,”amesema Beatrice.
Aidha,amemtaka Mkurungenzi wa Manispaa ya Ubungo kupitia michoro ya eneo hilo na kuweka mpangilio mzuri na kutambua ni ardhi ipi utunzwe kwa ajili ya matumizi ya baadae.
Katika hatua nyingine Chalamila amezipongeza taasisi za dini kwa mchango wake kwa kuisaidia serikali kuleta maendeleo kupitia sekta ya afya,elimu na barabara.
“Ni wazi mchango wa sekta binafsi katika kuleta maendeleo umeonekana wazi ni washukuru sana wadau wetu kutoka Kanisa la Watakatifu wa Kanisa la Yesu Kristo kwa kusaidia ujenzi wa shule ya msingi Msewe hasa kwa kuweka madarasa na vyoo vinavyoweza kutumiwa na wanafunzi wenye mahitaji maalumu hivyo ninyi wazazi leteni watoto wenu wenye mahitaji maalumu waje kupata elimu na si kuwafungia,”amesema Chalamila.



