Chalamila ataka mabadiliko soko la samaki Feri

akerwa na uholela wa wafanyabiashara

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amemtaka Meneja wa Soko la Feri Denis Mrema kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake abuni vyanzo vya vipya vya kuongeza mapato.

Pia, amemtaka kupitia upya sheria zilizopo kwa kushirikisha wafanyabiashara hili kupunguza kero kwa wafanyabiasha hao.

Chalamila ameyasema hayo alipotembelea soko la Feri na moja ya changamoto aliyokutana nayo ni soko hilo kukabiliwa na idadi kubwa ya wafanyabiashara zaidi ya 3000 huku uwezo wake halisia ni kuhudumia wafanyabiashara wapatao 1500 hadi 2000 pekee.

Amesema, Rais Samia ana nia njema na wafanyabishara hao wa soko la Feri na kuwataka kila mmoja anayefanya biashara katika Soko hilo kuwa mlinzi wa mwenzie hili idadi ya wafanyabishara iliyopo sasa ya zaidi 3,000 isiongezeke hadi pale Serikali itakapofanya maboresho ya Soko.

Chalamila amesema, amebaini uholela wa wafanyabishara, kukosekana kwa uaminifu miongoni mwa wafanyabishara kupitia kiwango cha mapato ambacho kinatakiwa kipatikane, ubovu wa miundombinu, sheria sio shirikishi hivyo ni wakati muafaka wa kuanza kupangana.

“Bado kuna uholela kila mmoja haelewi yuko wapi baadaye yanaibuka maugomvi kwa hiyo hili lazima tuje tuendelee kupangana upya angalau kusiwe na migogogro ya mara kwa mara,  jambo la pili ambalo nimeligundua baadhi yetu sio wa kweli kwenye mapato yanayotakiwa kuingia hapa,”amesema Chalamila.

Aidha, ameagiza kupunguza matumizi ya mkaa katika soko hilo ambayo huzalisha moshi na kuwataka  kuanza matumizi ya gesi asilia.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya IIala Edward Mpogolo akizungumza alisema  pamoja juhudi kubwa inayofanywa na Wilaya hiyo ziko changamoto kadhaa katika soko hilo ikiwemo migogoro kati ya Kanda  moja na nyingine, ukosefu wa friji la kuifadhia samaki kwa baadhi ya maeneo, wafanyabishara ni zaidi ya 3,000 na kuwepo kwa mchanga kando ya ferry hiyo ambapo awali meli za samaki zilikuwa zinatia nanga lakini  siku hizi haiwezekani.

“Hivyo ujio wako  Mkuu wa Mkoa,  imekuwa faraja kubwa na tupo tayari kukusikliza  na kupokea maagizo na maelekezo yako kwa masilahi mapana ya wafanyabishara katika soko hili.”Amesema Mpogolo

Kwa upande wa wafanyabiashara wa soko hilo Tausi Isaya ambaye ni mamalishe na Obed Samueli ambaye ni baba lishe,kwa nyakati tofauti wamesema, mfumuko wa bei ya vyakula uliopo kwa sasa unasababisha wasipate faida kwenye biashara wanazofanya, nakwamba pia kuna baadhi ya wafanyabiashara wa chakula kutoka nje ya soko hilo la Feri wanakwenda kufanyabiashara ndani ya soko hilo hali inayochangia wafanye biashara katika mazingira magumu.

 

Habari Zifananazo

8 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button