Chalamila: Takwimu za kuzaliwa, vifo muhimu kwa upangaji sera

DAR ES SALAAM: SERIKALI kupitia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila imesisitiza kuwa takwimu sahihi za vifo na kuzaliwa ni nguzo muhimu katika kupanga sera madhubuti za afya na maendeleo ya taifa.

Chalamila amsema hayo leo kwenye mkutano wa Kimataifa wa Mipango na Kubadilishana Uzoefu kuhusu Mfumo wa Usajili wa Sampuli (SRS).

Amesema Tanzania ipo katika harakati za kuimarisha mfumo wa usajili wa sampuli (SRS) kwa ushirikiano na taasisi za kitaifa na kimataifa.

Chalamila amesema Tanzania imeanza kupiga hatua katika kuimarisha takwimu sahihi za matukio ya vifo na vizazi kupitia miradi ya pamoja na taasisi kama Ifakara Health Institute (IHI) na Vital Strategies.

“Takwimu hizi hutuwezesha kupanga vizuri. Tukijua nani anafariki, wapi na kwa nini, tunaweza kuingilia kati mapema. Taarifa hizi ni muhimu kwa kila hatua ya kisera,” alisema.

Alitolea mfano wa tukio la mlipuko wa ugonjwa mkoani Kagera, ambapo uelewa mdogo wa jamii kuhusu utoaji wa taarifa za vifo uliathiri uingiliaji wa haraka wa wataalamu wa afya. Aliitaka jamii kushiriki kikamilifu katika kutoa taarifa hizi kwa maendeleo ya afya ya taifa.

SOMA ZAIDI

Chalamila: Ujenzi wa daraja Jangwani kuanza mwaka huu

Kwa upande wake, Dk Honorati Masanja, Mkurugenzi wa Ifakara Health Institute, alisema kuwa taasisi hiyo kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine kama Wizara ya Afya, RITA, NBS na BAKWATA, inatekeleza kwa mafanikio mfumo wa SRS unaolenga kutoa takwimu sahihi za vifo na kuzaliwa nchini.

“Changamoto kubwa ni kutokuwepo kwa mifumo ya serikali inayosomana kwa urahisi. Mara nyingi taarifa za vifo zipo, lakini haziwasilishwi kwa wakati kwenye taasisi husika,” alisema.

Aliongeza kuwa SRS inalenga kutoa picha halisi ya hali ya kiafya ya Watanzania kwa kutumia mbinu za kitaalamu zinazozingatia usawa na wakati.

Philip Setei, Makamu wa Rais wa Programu za Afya ya Umma na Mkurugenzi wa Maboresho ya Usajili wa Matukio Muhimu ya Kiraia (CRVS) lenye makao makuu New York, alisema kuwa juhudi hizi zitasaidia Watanzania kupata huduma bora kwa kuzingatia ushahidi wa kisayansi.

“Hatuwezi kupanga huduma sahihi bila kujua chanzo cha vifo. Takwimu hizi ni msingi wa kuokoa maisha kwa sera bora,” alisema Setei, ambaye pia alielezea uzoefu mzuri wa Tanzania katika kushirikiana kwenye miradi kama hii kwa zaidi ya miaka 20.

Setei alisisitiza kuwa nchi kama Msumbiji zimefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kuingiza takwimu za vifo katika mfumo wa kitaifa wa afya na sasa zinazalisha data za kuaminika kwa matumizi ya sera.

Sam Dolan, Ofisa Mwandamizi kutoka Bill & Melinda Gates Foundation, alisema taasisi yao ina imani kubwa na jitihada za Tanzania, na itaendelea kutoa msaada wa kifedha na kitaalamu katika kuboresha mfumo wa SRS.

Alisema Tanzania ni miongoni mwa nchi sita barani Afrika zinazopata ufadhili wa awali kutoka kwa taasisi hiyo katika kutekeleza mfumo wa SRS, sambamba na nchi kama Sierra Leone na Msumbiji.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button