MKURUGENZI Mtendaji wa shirika la umeme nchini (TANESCO) ,Maharage Chande amesema katika kuongeza ufanisi uwajibikaji na utendaji wa kazi Shirika la Umeme nchini TANESCO, wamedhamiria kumaliza changamoto ya umeme ifikapo mwezi June 2024.
Mkurugenzi huyo ameitoa kauli hiyo leo Julai 27, 2023 Dar es Salaam katika mkutano wa shirika hilo na wahariri wa vyombo vya habari na kusema changamoto ya umeme nchini itabaki kuwa historia kutokana na kukamilika kwa mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere litakalochangia uzalishaji umeme kwa wingi ambapo kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 90 hadi kukamilika kwake.
Aidha Mkurugenzi huyo amesema shirika hilo lina mpango wa kuja na mita janja ili kupunguza mchakato mrefu wa ulipaji umeme
“Mita janja zitawezesha mtu kuingiza umeme na sio lazima awe nyumbani kwake popote pale alipo anaweza kuingiza umeme, tulianza tathimini ya kuhama mfumo kutoka mfumo tuliopo sasa ya kwenda kwenye mfumo mpya wa mita janja na matokeo ya tathimini hiyo yalishatoka.
“zipo mita janja ambazo tunazijaribu na zinafanya kazi licha ya kwamba tumepata changamoto ya gharama kubwa ya matumizi yake , kwasasa tunaanagalia njia mbadala ambayo itapunguza gharama kwa watumiaji wetu” amesema Chande
Mkurugenzi wa huduma kwa wateja TANESCO Martine Mwambene amesema kuanzishwa kwa kurugenzi za mawasiliano ndani ya shirika hilo kumesaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto za wateja wao na sasa upatikanaji wa huduma zao hazimlazimu tena mteja kufika ofisini ili asaidike.
Mwenyekiti wa jukwaa la wahariri wa vyombo vya habari TEF Deodatus Balille ameleeza kuwa maboresho yanayoendelea kufanywa na shirika hilo yana tija kubwa katika utoaji wa huduma zake kwa wateja na ameshauri mfumo wa utendaji wa shirika hilo utumike pia katika taasisi zingine za Umma.
Kwa sasa mizani ya shirika la umeme nchini imeendelea kukua ambapo kwa mwaka wa fedha 2021/2022 shirika hilo limeweza kupata mauzo ya shilingi trilioni 1.8 na faida ya shilingi Bilioni 109 kwa mwaka 2022 na matarajio yao ni kukuwa zaidi.