Charles Hillary aagwa Dar, kukumbukwa kwa mengi

MWILI wa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu na Msemaji Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Charles Hillary umeagwa leo katika Kanisa la Anglikana la Mtakatifu Batholomayo, Ubungo, Dar es Salaam.
Viongozi, ndugu, jamaa na waumini mbalimbali wameshiriki ibada hiyo ya kumuaga iliyofanyika jana kanisani hapo ambapo wamemtaja Charles kuwa mtu aliyependa ibada na kujitoa katika kila jambo lenye manufaa.
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes alisema Charles alikuwa mhamasishaji na mstari wa mbele katika masuala yanayohusu umoja wa akina baba kanisani na alikuwa mtu mwenye kulipenda kanisa lake na kupenda ibada.
Alisema tofauti na watu wengine ambao hudhani umaarufu ni utoshelevu wa maisha na hawamuhitaji Mungu, ilikuwa tofauti kwa Charles kwani aliishi maisha ya kumtanguliza Mungu katika kila jambo, hakuweza kukosa ibada pale ambapo ratiba ilimruhusu.
“Amekuwa muumini wa kanisa hili mchango wake ni mkubwa katika kanisa hili. Kikawaida hapa kunakuwa na mashindano ya wanaume na wanawake kufanya mambo mbalimbali, kama huu msiba umekuwa mkubwa, umekuwa mkubwa zaidi kwa wanaume wa kanisa hili,” alisema Askofu Sosthenes.
Mwanahabari mkongwe, Abdallah Majula alisema Charles alikuwa mwanahabari aliyeifahamu vema lugha ya Kiswahili na alikuwa akitumia muda wake kuwasahihisha watangazaji walipokuwa wakikosea kutamka maneno kwa usahihi.
“Alikuwa ananiambia Majura wewe ni mtangazaji mzuri sana una sauti nzuri sana ila tatizo lako ni kutofautisha L na R na kila siku alikuwa ananipa mtihani huo,” alisema.
Majura alisema anamkumbuka Charles alivyokuwa mahiri katika utangazaji sambamba na kuandaa matangazo ya biashara alipokuwa akihudumu Redio One.
Alisema Charles alikuwa kiongozi aliyependa kuelekeza ili kujenga, sambamba na kuwaamini watumishi waliokuwa chini yake.
“Nakumbuka wakati anafariki Baba wa Taifa yeye alikuwa Mkuu wa Kitengo cha Habari na Matukio aliniambia Majura nakuamini na aliniamini kuongoza matangazo,” alisema.
Mwanahabari, Nevile Meena alisema Charles alikuwa mtu aliyependa kujishusha katika utendaji wake: “Akiwa pale Azam alikuwa yeye na Ivona ukimuangalia Charles na Ivona ni mtu na mzazi wake walivyokuwa wakitangaza unaweza ukadhani wana umri sawa katika taaluma,” alisema.
Meena alisema Charles alikuwa mtu anayependa kujifunza na mwenye maarifa mengi kuhusu mambo mbalimbali ambaye alikuwa hawezi kuingia kusoma habari bila ya kujiandaa.
Mkazi wa Ubungo na Mjumbe wa Mkutano Mkuu Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Dunstan Mapunda alisema kifo cha Charles ni pigo kubwa kwa kanisa la Anglikana na Wanaubungo kwa jinsi ambavyo alikuwa akijitoa katika ujenzi wa kanisa hilo.
Joshua Ezekiel naye alisema Charles alikuwa mtu mahiri hasa katika utangazaji wa mchezo wa mpira wa miguu, alisema alitangaza vipindi vingi lakini utangazaji wake wa mpira wa miguu ulikuwa hauna mfano.
“Ukisikiliza mpira utadhani upo uwanjani alikuwa na lafudhi nzuri anataja majina kwa ufasaha yaani alikuwa mtangazaji mzuri sana, si mpira tu hata vipindi vingine ila kwangu mimi utangazaji wake wa mpira ulikuwa unanivutia sana,” alisema.
Ibada hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa serikali wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye aliongoza ukusanyaji wa michango kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo.
Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete akiwa nyumbani kwa Charles, Kibamba, Dar es Salaam, kutoa pole alisema alifahamiana na Charles miaka mingi akiwa mtangazaji maarufu wa mpira, Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji Tanzania (Redio Tanzania wakati huo) na akiwa maarufu kwa kipindi cha Charanga na hata alivyoenda nje ya nchi na kurudi kisha kwenda Zanzibar wamekuwa wakikutana na kukumbushiana mambo ya zamani.
“Moja ya kitu ambacho amekuwa ananifanyia na naendelea kumshukuru alikuwa ananirekodia nyimbo za charanga na mara ya mwisho tulikutana Zanzibar aliahidi ananitengenezea nyingine, ni mtu mzuri, mwema, mtu mcheshi sana, tumepoteza mwandishi wa habari nguli mwenye weledi wa kiwango cha juu. Tumepoteza raia wa Tanzania ambaye ni Mzalendo wa dhati,” alisema Kikwete.
Baada ya ibada hiyo iliyofanyika Ubungo, mwili wa Charles ulisafirishwa kwenda Zanzibar ambapo unatarajiwa kuagwa leo katika Viwanja vya Mapinduzi Square (Kisonge) na kuzikwa saa 10 jioni katika makaburi ya Mwanakwerekwe, Mkoa wa Mjini Magharibi.