Chatanda aahidi kufuata dira anayoitaka Samia

Mwenyekiti mpya wa UWT, Mary Chatanda

UONGOZI mpya wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) umeahidi kuongoza jumuiya hiyo kwa kuzingatia dira aliyoitoa Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Mwenyekiti mpya wa UWT, Mary Chatanda alisema katika kipindi cha miaka mitano, wataenda na dira ambayo ameitoa mwenyekiti wa chama kupitia mkutano wao wa juzi.

“Uongozi huu tunashukuru mwenyekiti wa taifa ametuonesha dira na mwelekeo wa nini tunachotakiwa kufanya kama jumuiya. Tunachoahidi ni kwamba tutafuata dira na mwelekeo na mipango kazi ambayo tayari ilishaandaliwa kwa mustakabali wa jumuiya,” alisema Chatanda aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Korogwe Mjini mkoani Tanga.

Advertisement

Chatanda pia aliwashukuru wajumbe na wasimamizi wa uchaguzi kwa kuufanya uwe wa huru na haki huku utulivu mkubwa ukitawala kwenye upigaji kura.

“Tunawashukuru sana kwa uchaguzi huu uliofanyika kwa amani na utulivu mkubwa, tunawashukuu wasimamizi kwa kusimamia kwa uhuru na haki,” alisema mwanasiasa huyo mzoefu aliyewahi pia kuwa Katibu wa CCM Mkoa.

Makamu Mwenyekiti UWT Taifa, Zainab Khamis Shomari alimshukuru Rais Samia kwa kuonesha mwelekeo wa nini kinatakiwa kufanyika ili jumuiya isonge mbele.

Pia aliwashukuru wajumbe waliowaweka madarakani na kuahidi kuwa watatoa ushirikiano bila ubaguzi wowote.

“Niwashukuru wajumbe wote mliotupigia kura na msiotupa kura, tuahidi ushirikiano wa hali ya juu. Mchakato huu haukuwa mwepesi, katika safari kuna mabonde na milima, lakini hatimaye unafika salama unapotaka kwenda,” alisema Shomari.

“Sisi viongozi tuliochaguliwa tupo tayari kufanya kazi kwa kushirikiana na wanachama wote wa UWT bila ubaguzi, pia tuko tayari kushirikiana na wote ambao watatoa ushirikiano hatuna tatizo sababu hakuna uchaguzi usio na makundi,” alisisitiza.

Alitoa rai kwa wanachama kuvunja makundi yaliyokuwapo na kushirikiana kuendelea na kazi.

“Tuliochaguliwa leo (juzi) ndio viongozi wa UWT hii ambao tutaongoza miaka mitano, kwa mantiki hiyo natangaza wazi kwamba wale wote waliokuwa wakitushabikia au wenye mapenzi ya dhati na sisi, sisi tunawashukuru lakini tunachokiomba tuimbe na tusimame na jumuiya na chama.”

Aliyekuwa Mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudentia Kabaka aliwahakikishia wajumbe wa mkutano huo kuwa licha ya kutokutosha kura, ana amani na atashirikiana vizuri na viongozi wapya.

“Nawaomba tutakapoanza kipindi hiki cha miaka mitano tuendelee kuwa na utulivu ndani ya jumuiya yetu kama tulivyokuwa kipindi kilichopita,” alisema mwanasiasa huyo ambaye kitaaluma ni mwalimu.

“Tumeambiwa wanawake na jumuiya hii ndio nguzo ya chama hivyo hatutarajii kusambaratika kutokana na tofauti zetu za uchaguzi zinazojitokeza, hivyo wakati naenda kupumzika nipo tayari kushirikiana nanyi.”

Akizungumza kabla ya kutangazwa matokeo, msimamizi wa uchaguzi huo, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda alisema kamati aliyoiongoza ilihakikisha inatenda haki kwa wagombea wote.