China kufadhili mradi wa SGR Isaka – Mwanza

DAR-ES-SALAAM : NAIBUWAZIRI wa Fedha, Hamad Hassan Chande, ameishukuru Serikali ya China kupitia Shirika la Bima la SINOSURE kwa kudhamini mkopo wa kibiashara wa dola za Marekani milioni 559 kwa ajili ya ujenzi wa kipande cha tano cha Reli ya Kisasa (SGR) kutoka Isaka hadi Mwanza, kufuatia mkataba uliosainiwa Oktoba 21, 2024.
Chande alitoa shukrani hizo wakati wa kikao cha majadiliano kati ya Ujumbe wa Tanzania, ukiongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, na Ujumbe wa China, ukiongozwa na Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China, Tang Wenhong, kilichofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam.
Aidha, aliiomba China kuangalia uwezekano wa Shirika la SINOSURE kushiriki pia katika kudhamini kipande cha sita cha SGR kutoka Tabora hadi Kigoma, chenye makadirio ya gharama ya dola bilioni 2.3, ambapo dola bilioni 1.1 zinatarajiwa kutoka kwa Taasisi za Fedha za Maendeleo (DFIs).
Chande pia alieleza kuwa ushirikiano wa karibu kati ya Tanzania na China umechangia upatikanaji wa dola milioni 108.6 kwa Mradi wa Kuongeza Wigo wa Mawasiliano Vijijini – Awamu ya Kwanza, na dola milioni 270.3 kwa Mradi wa Usafirishaji Umeme wa kV 400 kutoka Dar es Salaam hadi Arusha.
Amesema uchumi wa Tanzania unaendelea kuimarika kutokana na uwekezaji katika miundombinu, mazingira mazuri ya biashara, na utulivu wa kiuchumi. SOMA: Mradi wa SGR Isaka – Mwanza wabadilisha maisha ya wananchi
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Biashara wa China, Tang Wenhong, alisema China itaendelea kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kidiplomasia na Tanzania kwa manufaa ya wananchi wa mataifa yote mawili.