Chissano ampongeza Samia kuthamini Kiswahili
RAIS mstaafu wa Awamu ya Pili wa Msumbiji, Joachim Chissano amesema utoaji wa Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu, ni matokeo ya juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan kuthamini, kukuza na kuendeleza Lugha ya Kiswahili nchini.
Alitoa kauli hiyo juzi mkoani Dar es Salaam alipokuwa mgeni katika hafla ya utoaji tuzo hiyo kwa mwaka 2023 iliyoandaliwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na kuratibiwa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) kwa washiriki kutoka Tanzania Bara na Zanzibar katika nyanja za ushairi na riwaya.
Hamis Kibari aliyekuwa Mhariri Msanifu katika gazeti la HabariLEO, aliibuka mshindi wa kwanza kwa riwaya na kupata cheti, ngao na Sh milioni 10 kupitia muswada wake wa ‘Gereza la Kifo’ akifuatiwa na Dickson Damas aliyepata cheti na Sh milioni saba kupitia muswada wa ‘Kigodoro Kimeniponza.’
Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, serikali itagharamia uchapaji wa miswada iliyopata ushindi wa kwanza katika riwaya na ushairi na kuisambaza katika shule na maktaba nchini. Rais Chissano aliwataka Watanzania kumsaidia Rais Samia na kumpa ushirikiano zaidi kuendeleza Kiswahili na mambo mbalimbali ya kitaifa kwa ujumla. “Msaidieni Rais Samia, anafanya kazi hii kwa makini sana…” alisema Chissano na kuongeza: “Utoaji wa tuzo hii ni kuendeleza amali muhimu ya Kiswahili nchini Tanzania na katika Afrika kwa jumla.”
Kwa mujibu wa Chissano, Kiswahili nyumbani kwake ni Tanzania hivyo Watanzania hawana budi kukilinda na kukitumia kwa tija kama lugha adhimu. “Kiswahili ni lugha yetu Afrika, tukilinde kukikuza na kukipa heshima kwa kukitumia katika elimu, siasa na masuala mengine ya kijamii,” alisema Rais mstaafu huyo.
Aliwapongeza Watanzania kwa kuenzi mchango wa Nyerere katika kukuza Kiswahili, na pia kupongeza uhusiano wa kihistoria baina ya Tanzania, Msumbiji na nchi nyingine uliowezesha kupatikana kwa ukombozi wa nchi za Afrika.
Akizungumzia uhusiano huo, Chissano alisema: “Waziri amenisifia sana katika harakati za ukombozi, lakini mafanikio yangu yalitokana na mafunzo niliyoyapata kutoka kwa viongozi wa Tanzania na umma wa Watanzania kwa ujumla….” “Hata Kiswahili, tulijifunza kupitia hotuba zake (Nyerere) maana alitumia Kiswahili chepesi kwa kuwa alikuwa mwalimu aliyewezesha hata wengine tusiojua Kiswahili tukielewe…” Katika kumkaribisha Chissano, Profesa Mkenda alimpongeza na kumshukuru kwa kuja nchini kukienzi Kiswahili na kumuenzi Nyerere aliyeshirikiana katika ukombozi wa nchi za Afrika.
Alisema ili kuchochea na kuendeleza uandishi bunifu, serikali inaangalia uwezekano wa kuanza kununua na kusambaza vitabu vinavyoandikwa nchini vikiwamo vya marais wastaafu na Watanzania wengine. Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu ya Mwaka 2023, Profesa Penina Mlama, miswada 283 iliwasilishwa ikihusisha 193 ya ushairi, 85 ya riwaya na mitano ya nyanja ambazo hazikuhitajika.