Chongolo ampa waziri siku 10 kilio cha maji Uhambingeto

KATIBU Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo ametoa siku 10 kwa Waziri wa Maji, Juma Aweso kufika katika kata Uhambingeto iliyopo Wilaya ya Kilolo Mkoa wa Iringa kushughulikia changamoto ya ukosefu wa maji iliyoripotiwa na diwani wa kata hiyo.

Chongolo amepewa malalamiko hayo alipofanya ziara yake leo Mei 31, 2023 katika kata hiyo huku baadhi ya wananchi wakiangua vilio na kuishutumu Kampuni ya Mshamindi Construction Ltd kuwa sababu ya wao kuendelea kukosa huduma ya maji safi na salama.

Diwani wa kata hiyo, Tulinumtwa Mlangwa alisema wananchi wa kata yake walipata matarajio ya changamoto ya maji katika kata yao kushugulikiwa baada ya Julai mwaka jana kampuni hiyo kupewa tenda ya kufanya kazi hiyo.

Huku akilia kwa uchungu na kupiga magoti diwani huyo alimwambia Chongolo mradi huo wa thamani ya Sh bilioni 2.1 ulipaswa kukamilika Februari mwaka huu kabla mkandarasi huyo hajaongezewa miezi mingine minne inayoisha Juni, mwaka huu.

Pamoja na kuongezewa muda, diwani huyo alisema taarifa zinaonesha mkandarasi huyo amekwishalipwa malipo ya awali ya zaidi ya Sh bilioni 1.3 huku kazi iliyofanywa ikiwa ni asilimia 25 tu.

“Mheshimiwa Katibu Mkuu hakuna kazi yoyote inayoendelea na matumaini ya wananchi wangu kupata huduma ya maji inayoyoma, sisemi haya ili nichaguliwe tena; nalia kama mwakilishi wao kwasababu najua changamoto hii ya maji inavyotutesa hususani wanawake,” alisema.

Hisia zake zikizua vilio toka kwa wananchi wengi, alisema wanalazimika kuendelea kutumia kwa pamoja na wanyama maji ya kwenye madimbwi kwa matumizi yao ya majumbani.

Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Justine Nyamoga alisema gharama ya maisha ya wananchi wa kata hiyo yameongezeka kwani ili wapate maji safi ya kunywa wanalazimika kununua ndoo moja ya lita 20 kwa hadi Sh 5,000.

Bila kumtaja mkanadarasi huyo Nyamoga alishukuru ujio wa Katibu Mkuu katika kata hiyo akisema utasaidia mradi huo unaotarajiwa kuhudumia wananchi 11,900 kupatiwa ufumbuzi.

Huku mradi huo ukionesha umetekelezwa kwa asilimia 25 tu, taarifa inaonesha ujenzi ambao haujafanyika ni pamoja na wa tenki, vituo 14 vya maji na utandazaji wa mabomba.

“Yaelekea muhusika wa kampuni hii ni mtu anayejiamini sana ndio maana mradi huu hauendi pamoja na kwamba Rais Dk Samia Suluhu Hassan ametoa fedha zake zote kwa ajili ya utekelezaji wake,” alisema.

Pamoja na jina la mkandarasi huyo kutowekwa wazi baadhi ya watu walio jirani na mradi huo (hawakutaka kutaja majina yao) walisema inamilikiwa na mmoja wa wabunge wa bunge la Jamuhuri ya Muungano Tanzania (jina linahifadhiwa).

Akimtaka Waziri wa Maji kufika katika kata hiyo ndani ya siku 10, Chongolo alisema; “CCM haiwezi kukubali fedha zitolewe na serikali yake halafu mradi usitekelezwe.”

Akiukataa mradi huo alisema wananchi wa kata hiyo hawawezi kukosa huduma ya maji tu kwasababu ya changamoto ya mkandarasi.

“Hakuna kulindwa Mkandarasi. Kama kuna mtu analeta gizagiza kwa fedha zinazotolewa kwa ajili ya wananchi, mimi nina winchi la kumnyanyua,” alisema na kuongeza hakuna mtu wa kupinga matumizi ya fedha zinazotolewa na Rais kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.

Alishauri mradi huo utekelezwe kwa kutumia mafundi wa kawaida (Force Account) na akatoa miezi mitatu hadi Septemba 30, mwaka huu wananchi wawe wamepata maji.

“Na kabla ya mradi huu kukamilika nitaleta matenki makubwa mawili ya ujazo wa lita 10,000 kila moja ili muanze kusambaza maji kwa wananchi wakati ujenzi uliobaki ukiendelea,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button