CONGO : Wanajeshi 75 kizimbani kukimbia mapigano

CONGO : WANAJESHI  75 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wanatarajiwa kupandishwa kizimbani leo kwa tuhuma za kukimbia mapigano, kufuatia mashambulizi ya waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda katika jimbo la mashariki la Kivu Kusini.

Taarifa iliyotolewa Jumapili na ofisi ya mwendesha mashtaka wa kijeshi inasema kuwa askari hao wanakabiliwa na mashitaka ya vurugu dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na mauaji, uporaji, na ubakaji.

Wanajeshi hao walikamatwa baada ya kuondoka kwenye mji wa Nyabibwe, ambao ulikuwa umeingiliwa na waasi wa M23. Shirika la habari la Reuters linaripoti kuwa askari hao wanashitakiwa kwa makosa ya mauaji, uporaji, ubakaji, na uasi. SOMA: CONGO: Mapigano yameanza tena kusini mwa Kivu

Umoja wa Mataifa umetoa taarifa ikieleza kuhusu ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, ikiwa ni pamoja na unyongaji, ubakaji wa magenge, na utumwa wa kingono, uliofanywa baada ya msako mkubwa wa M23 mwishoni mwa mwezi Januari, ambao ulisababisha kutekwa kwa mji wa Goma, mashariki mwa DRC.

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa iligundua kuwa, pamoja na waasi wa M23, askari wa serikali na wanamgambo wanaounga mkono serikali wamehusika katika ukiukaji huo wa haki za binadamu.

Hata hivyo, Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo haijatoa ripoti rasmi kuhusu hatua dhidi ya vikosi vyake, lakini imeutaka Umoja wa Mataifa kuchunguza ukiukaji wa haki za binadamu unaofanywa na waasi wa M23 na serikali ya Rwanda.

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button