CRDB, Costech kutumia bilioni 2.3/- kuwezesha biashara

DAR ES SALAAM – BENKI ya CRDB na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) wamesaini mkataba wa Sh bilioni 2.3 kwa ajili ya kuziwezesha biashara changa za vijana.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda alishuhudia kusainiwa kwa makubaliano hayo yakiwa ni sehemu ya programu ya IMBEJU kupitia dirisha lake la IMBEJU BUNI yakilenga kuwasaidia vijana wabunifu nchini kupata elimu ya fedha na mitaji nafuu ya kukuza biashara zao.

“Hii ni hatua ya kupongezwa inayochochea ukuaji wa uchumi wa ubunifu. Ushirikiano huu ni jibu la changamoto ya kukosekana kwa ufadhili kwa vijana wabunifu na ni kielelezo cha juhudi za serikali kujenga uchumi shindani wa viwanda wenye ubunifu,” alisema Profesa Mkenda.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Benki ya CRDB, Tully Mwambapa alisema ushirikiano huo unaakisi dhamira ya Benki ya CRDB kushiriki kujenga uchumi jumuishi.

“Tangu kuanzishwa kwa Programu ya Imbeju Machi 2023, tulilenga kuwafikia vijana na wanawake waliopo pembezoni na kuwapa fursa za kifedha. Kupitia mkataba huu, tunatarajia kuwafikia vijana zaidi ya 1,000 na kuwapa mitaji wezeshi, mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha ili waweze kuendesha biashara endelevu kwa mfumo rasmi hivyo kuwa rahisi kwao kukua zaidi,” alisema Tully.

Katika kipindi hiki cha ushirikiano kati ya Benki ya CRDB na Costech, zaidi ya vijana 700 wabunifu wamefikiwa na kuwezeshwa kupitia dirisha la Imbeju Buni ambalo ni mahususi kwa ajili ya wabunifu wenye biashara changa kwa kuwapa mafunzo na mitaji wezeshi ya thamani ya takribani Sh bilioni tano.

PIA SOMA: TADB yaipa serikali gawio bil 6/-

Katika utekelezaji wa mkataba uliosainiwa kutakuwa na kamati yapamoja ya usimamizi kati ya Benki ya CRDB, taasisi ya benki hiyo, Costech kwa ajili ya kufanya tathmini, ufuatiliaji, na usimamizi madhubuti wa utekelezaji kuhakikisha kunakuwa na uwazi wa kutosha kulifikia lengo lililowekwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu alisema wanaendelea kujenga mazingira wezeshi kwa vijana kubuni na kustawi kibiashara. “Ushirikiano huu na CRDB Bank Foundation ni muendelezo wa safari tuliyoianza mwaka 2023, na sasa tunaongeza msukumo zaidi kufanikisha ndoto za vijana wengi,” alisema.

 

Habari Zifananazo

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Back to top button